Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu viashiria vya mtoto anayeficha siri ya udhalilishaji

Wed, 28 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nimekuwa nikishughulika na watoto wanaokumbana na masaibu ya udhalilishaji. Ingawa sina takwimu sahihi, nafahamu, idadi ya watoto wanaoishi na maumivu haya inazidi kuongezeka. Sehemu ya tatizo ni sisi wazazi, walezi, walimu na watu wengine tunaoishi na watoto kutokufahamu viashiria vya mtoto anayepita kwenye wakati mgumu lakini hana ujasiri wa kueleza yanayomsibu.

Wakati mwingine haya yote yanatokana na ukweli kwamba hatuko karibu na watoto na hivyo hatuwafanyi wajisikie huru kutuambia yale yanayoendelea kwenye maisha yao ya faragha. Pamoja na upungufu huo, bado sisi kama walinzi wa kwanza wa mtoto, ni muhimu kujifunza viasharia vya mtoto anayeishi na siri ya udhalilishaji.

Kwanza ni kuanza kujengeka kwa tabia ya hofu isiyo ya kawaida. Uzoefu unaonyesha kuwa mtoto anapodhalilishwa na mtu wake wa karibu, mara nyingi hutishwa sana. Ipo mifano mingi ya watoto kuonywa kuwa siku wakisema kinachoendelea, mama au ndugu zao wa karibu wangeuawa. Mdhalilishaji hufanya hivi ili kujilinda na fedheha ya kufahamika kwa uchafu wake.

Lakini kwa upande mwingine, mtoto hujikuta na kazi kubwa ya kuficha siri inayomzidi umri. Matokeo ya jitihada za kuishi na maumivu asiyopaswa kuyasema ni kujikuta anakuwa na hofu isiyoelezeka. Mtoto huogopa vitu ambavyo kwa hali ya kawaida usingetarajia vimwogopeshe. Mfano, mtoto anaposikia mama au ndugu wa karibu anakwenda kukutana na mtu fulani, au anakwenda mahali fulani, mtoto anaogopa na hata kulia kabisa. Katika mazingira kama haya, iko haja ya kufanya uchunguzi zaidi. Inawezekana huko asikotaka uende ndiko anakoishi mdhalilishaji.

Aidha, hutokea wakati mwingine mtoto akaanza kuwaogopa watu fulani aliokuwa amewazoea. Mfano, mnaishi na ‘anko’ wake hapo nyumbani lakini ghafla anaanza kumchukia. Inawezekana pia akawa ni mwalimu wake au mtu mwingine wa karibu. Hofu ya namna hii inaweza kuwa dalili ya kitu kinachoendelea kwa siri ambacho hata hivyo mtoto hana ujasiri wa kukisema. Usipuuze.

Lakini pia wapo watoto wasioonyesha wasiwasi uliopindukia lakini wanabadilika na kukosa amani. Kwa mfano mtoto alikuwa mchangamfu lakini ghafla anaanza kuwa mpweke, hataki kukaa na watu, anajistukia mara kwa mara. Wakati mwingine anaweza kuanza kupoteza uzingativu anapofanya shughuli zinazohitaji umakini. Hizi ni dalili za hatia anayojisikia ndani yake lakini pengine hana ujasiri wa kusema. Inawezekana ametishwa au anajua akisema kilichotokea atabebeshwa lawama. Chukua hatua.

Kwa upande mwingine, athari inaweza kuanza kuonekana kwenye maendeleo yake shuleni. Mara nyingi shauri ya kubeba mzigo mzito moyoni, mtoto hujikuta akitumia muda mwingine akijalaumu, akijiuliza afanye nini kujinasua, itakuwaje siku mambo yakifahamika. Mchanganyiko wa mambo kama haya unaweza kuathiri sana uzingativu wake masomoni. Unapoona mtoto anashuka kitaaluma bila sababu za msingi, inawezekana kuna mambo yanayoendelea unayohitaji kuyachunguza na kumpa msaada mapema. Je, tufanye nini kumsaidia mtoto mwenye dalili hizi?



Chanzo: mwananchi.co.tz