Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Eneo la ujenzi wa chuo lazua utata

Eneo Pic Data Eneo la ujenzi wa chuo lazua utata

Wed, 28 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakati wananchi wa Mtaa wa Kitelela wakisubiri fidia kupisha ujenzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), imeelezwa kuwa chuo hakina nia tena ya kuendeleza eneo hilo lenye eka 986.

Awali, Serikali ilitangaza kulitwaa eneo hilo kwa ajili ya kujenga Chuo cha Usafirishaji (NIT) na ingelipa fidia Sh7.8 bilioni kwa wananchi kupisha ujenzi, huku wakiamuriwa kutofanya maendelezo yoyote.

Mwananchi iliibua sakata hilo baada ya malalamiko ya wananchi na wakati huo Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa aliahidi kulipa ndani ya muda mfupi fedha hizo.

Hata hivyo, chuo hicho kimeandika barua ya kuliachia eneo hilo kwamba hawalihitaji tena baada ya kulishikilia kwa miezi 21 na kuzuia wananchi wasifanye maendelezo.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Profesa Mganilwa, hawana nia ya kuendelea na ardhi hiyo kwa madai wamepata eneo lingine mkoani Tabora lililokuwa chini ya Shirika la Reli Tabora kwa ajili ya kujenga kituo atamizi cha mafunzo.

Katika barua hiyo kumbukumbu namba BC.221/306/01 -A/55 ya Novemba 2022, NIT imeeleza changamoto ya fedha imesababisha kurudisha eneo hilo kwa wananchi.

Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Gabriel Migire alithibitisha kuruhusu eneo hilo kwa barua ya Novemba 17, 2022 DA.293/295/01/86 kwamba hawana shida na eneo hilo tena.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule alikiri kufahamu sakata hilo, lakini akasema hajapokea barua za kuelekeza kuwa eneo hilo limeachiwa, licha ya nakala kuwa zimenakilishwa katika ofisi yake.

Senyamule alisema bado anapata kigugumizi cha kulisemea jambo hilo na kuahidi kulifuatilia ili kujua ukweli.

“Hilo ni jambo la kawaida, lakini tutakaa na wananchi na tutajipanga, kwa sasa halijafika mezani kwangu, nitalifanyia kazi litakapofika, na kuhusu fidia yote tutayafanyia kazi kutokana na sheria na taratibu zilivyo baada ya kushauriana na wataalamu wangu, lakini tutapata mwafaka mzuri,” alisema Senyamule.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru aliomba jambo hilo lizungumzwe na Mkuu wa Idara ya Ardhi ambaye licha ya kutoa mawasiliano, lakini mara zote simu zake hazikupatikana na hata mwandishi alipokwenda ofisini alielezwa kuwa yuko nje ya ofisi kwa majukumu.

Chanzo: Mwananchi