ELIMU ya Afya ya uzazi inayojumuisha elimu ya uzazi wa mpango, elimu ya mabadiliko ya mwili kwa mtoto wa kike, maendeleo ya wajawazito sambamba na elimu ya utuamiaji wa njia za kuzuia mimba, kwa siku za hivi karibuni imeonekana kuwekewa msisitizo kwenye jamii.
Pia hali hiyo, iko shuleni ili kupunguza adha ya mimba za utotoni pamoja na vifo vya mama na mtoto.
Elimu hiyo, inayotolewa na mashirika mbalimbali chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikitolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari kwa maana ya televisheni, redio na magazeti, mitandao ya kijamii, vipeperushi pamoja na matamasha kwenye maeneo tofauti.
Kwa namna ya kipekee, imeonekana kuamsha uelewa wa jamii juu ya mstakabari wa afya ya uzazi hasa kwa watoto wa kike ambao ndiyo wametajwa kuwa waathirika wakubwa wa madhara yatokanayo na kukosa elimu ya afya ya uzazi ambapo wameonekana kupachikwa mimba za utotoni na pengine kukatisha ndoto zao za kuendelea na masomo.
Kwa nyakati tofauti, waathirika wakubwa wa mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia wametajwa kuwa watoto wa kike wenye umri kuanzia miaka 14, kwa mjibu wa tafiti zilizofanywa na mashirika mbalimbali yanayopigania haki za wanawake na afya ya uzazi ikiwemo Shirika la Mradi wa Usimamizi wa Elimu ya Uzazi wa Mpango na Afya ya Uzazi nchini (AFP & SH), wameeleza kundi linalotakiwa kuangaliwa zaidi sasa ni kuanzia miaka 10-24,ndiyo kundi lenye uhitaji mkubwa wa elimu ya kijinsia na afya ya uzazi.
AFP & SH, wanatanabaisha kuwa iwapo elimu ya kijinsia na elimu ya afya ya uzazi, itawafikia watoto wa kike wakiwa katika hatua za awali za ukuaji hasa miaka hii, itawasaidia kushinda vita ya ukatili wa kijinsia na changamoto za afya ya uzazi ambazo nyingi zimeonekana kusababishwa na kutokujitambua kwa watoto wengi wa kike.