Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ERASTO KADUMA; Mbunifu aliyeishia kidato cha tatu akitamani PhD

09eb1d57b9034a2f5ab1180ff353db76 ERASTO KADUMA; Mbunifu aliyeishia kidato cha tatu akitamani PhD

Thu, 18 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

“CHANGAMOTO za kiafya ndizo zilizonifanya niishie kidato cha tatu, badala ya kuhitimu kidato cha nne… Hata hivyo, baada ya hapo, nilijiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha Jakalanda kilichopo Mbeya na kuhitimu mwaka 1997 katika fani ya motor vehicle (ufundi wa magari).

“Kimsingi, hati ya manunuzi ya shamba na hati niliyonunua kiwanja cha nyumba kikiwa na hati ya kumiliki, zimenisaidia kupata mikopo midogo kutoka taasisi za fedha kwa ajili ya utafiti na ubunifu wangu…

“Kupitia vyuma chakavu vikiwemo vipuri vya magari, mashine na mitambo mbalimbali, nimefanikiwa kiviunganisha na kupata mtambo wa kukamua mafuta ya mimea hasa, alizeti.”

Ndivyo anavyosema Erasto Kaduma (48), mkazi wa Mtaa wa Sido mjini Njombe anayefanyia shughuli zake katika eneo la Parking ya Magari mjini Njombe.

Kaduma anasema hayo mbele ya umati wa wajasiriamali na wanufaika wa urasimishaji ardhi na makazi waliokutana na Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) mjini Njombe hivi karibuni.

Anasema: “Kwa kweli kwa kazi hizi za kibunifu tunazofanya, ufike wakati serikali itutambue na kutambua ubunifu wetu ili hata tupewe shahada maalumu za udaktari; tuwe madaktari wa PhD kwa heshima hata kama si kupitia mtiririko kamili wa mfumo wa kawaida wa elimu nchini.

“Unajua na sisi wabunifu tunatamani kupata shahada za utambuzi za udaktari za heshima kutokana na mchango wetu kwa jamii kupitia kazi tunazofanya… Kuna watu hawajasoma sana, lakini wamefanya ubunifu mkubwa na umuhimu wa kisayansi wanaostahili kutambuliwa na kupewa hata heshima ya udaktari ili waongeze mchango kwa taifa,” anasema.

Mbunifu huyo katika mazungumzo ya pamoja na mkewe Elizabeth Mbuji, anasema serikali ikiwatambua na kuwawezesha, itaokoa fedha nyingi zinazotumika kuagiza baadhi ya vipuri kutoka nje ya nchi kwa kuwa wapo Watanzania wenye uwezo wa kuvizalisha kwa ubora, kupitia vyuma chakavu vinavyopatikana nchini.

Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Mkurabita waliotembelea mashine ya mbunifu huyo hivi karibuni wakiongozwa na Mwenyekiti, Daniel Ole Njoolay, wanawapongeza Kaduma na mkewe kwa ubunifu huo wa kijasiriamali na kusema, watu kama hao wana mchango mkubwa katika kuipeleka kwa kasi Tanzania katika uchumi wa viwanda.

MKE NI MUUGUZI ALIYEGEUKA ‘MHANDISI’

Wakati Kaduma anasema hayo, mkewe, Elizabeth Mbuji ambaye kitaaluma ni muuguzi, anasema mbele ya Kamati ya Uongozi ya Mkurabita: “Nilikuwa nesi, lakini sasa mimi ndiye ‘injinia’ wa mashine hii na ninaipenda sana kazi hii.”

Mintarafu sababu za kuhama kutoka uuguzi na kuwa injinia wa mashine, Elizabeth anasema: “Huyu mume wangu hakuwa anapenda kazi yangu ya unesi kutokana na ile hali ya siku nyingine kukesha nje ya familia hivyo, mwanzoni niliingia katika mambo ya ujasiriamali; nilipenda sana zao la alizeti na namna ya kukamua na kuuza mafuta.”

Anasema hali hiyo, ilimfanya kuwa karibu kikazi na mumewe katika kazi za mashine aliyobuni Kaduma, lakini tatizo likawa ikipata hitilafu, wanalazimka kutafuta fundi kutoka Makambako hali iliyowagharimu fedha nyingi kumlipa na kumhudumia akiwa hapo (Njombe).

“Ikawa fundi akija, ninakuwa karibu naye sana, mara ananituma hiki, mara hiki, lakini na mimi, ninapenda kumuuliza tatizo ni nini na huku nikiangalia kwa makini namna anavyotengeneza… Nikaanza kuwa najaribu mwenyewe tatizo kama hilo linapotokea na bahati zuri, kila nilipojaribu nilifanikiwa kutengeneza mashine kama anavyofanya fundi.”

Kwa mujibu wa mwanamke huyo, tangu hapo akawa ndiye fundi wa mashine yao na hivyo, kuokoa fedha ambazo wangezitumia kwa fundi.

SAFARI YA ELIMU ILIVYOKWAMA

Safari ya elimu ya sekondari aliyoianza Kaduma mwaka 1991 katika Shule ya Sekondari ya Njombe, iligonga mwamba mwaka1993 akiwa kidato cha tatu. “Nilipata changamoto ya kiafya (tunaihifadhi) hivyo, nikashindwa kuendelea hadi kidato cha nne.

“Ndipo nikajiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Jakalanda kilichopo Mbeya tangu mwaka 1995 na kuhitimu mwaka 1997 katika fani ya ‘motor vehicle yaani, umakanika sambamba na mafunzo ya udereva na kupata vyeti kutoka Veta (Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi).”

Kaduma anasema kati ya mwaka 2003 na mwaka 2016, alikuwa mfanyakazi aliyeajiriwa na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe akiwa fundi mchundo na dereva wa mitambo.

“Lakini kwa kukosa kukamilisha elimu ya sekondari yaani kidato cha nne, tusio na vyeti vya ‘form four’ tukatumbuliwa mwaka 2017… Hata hivyo, wakati naendelea na kazi, nilikuwa naendelea kufanya ubunifu wa vitu mbalimbali na mtaji wa ubunifu wangu niliupata kupitia sehemu ya mshahara wangu…,” anasema.

KADUMA ALIVYOANZA UBUNIFU

“Ubunifu wangu uliuanza nilipokuwa nimeajiriwa na halmashauri na huko, ndipo nilipopata mtaji kupitia mshahara niliokuwa nikipata ulioniwezesha pia kupata nyumba na mashamba.

“Nilikuwa naangalia changamoto za watu, mfano shida za vipuri, hata katika mashine za kukamua mafuta ya alizeti; ndipo nikafikiria na kubuni mashine rahisi ya kukamua alizeti.”

Anasema katika ubunifu wake, alitumia vipuri vya mashine na vyombo mbalimbali vikiwamo vya trekta alivyovipata kwa wauzaji wa vyuma chakavu kwa bei ya chini.

“Kwa mfano, kifaa cha kuongeza nguvu ya treka kwenye tairi nilikinunua kwa takriban Sh 700,000. Kifaa hiki kikiwa kipya, dukani huuzwa kwa kati ya Sh milioni tano hadi milioni sita….”

“Nilifikiria na kuanza kutengeneza reli (msingi) ambao ni sehemu ya kuweka vifaa hivyo kikiwemo cha kuongeza nguvu (kigeuza mwendo) kinachopeleka mwendo kwa njia ya propelashafti kwenye mtambo unaokamua mafuta,” anasema Kaduma.

Anafafanua: “Kazi ya kifaa hicho ni kuchukua mwendo kutoka kwenye mota na kuubadili kwa kuupunguza hadi kwenye mtambo kwa kadiri ya kasi ya mzunguko kwa dakika…”

ALIPOFIKIA

Kwa mujibu wa mbunifu huyo wa mashine kupitia kuunganisha vyuma chakavu, hadi sasa amekwishatengeneza mashine tatu; mbili zimechukuliwa na wenzake waliokuwa wanachangaia kwa namna mbalimbali ununuzi wa vifaa vya kutengeneza mashine hizo na sasa amebakiwa na moja anayofanyia kazi.

“Mmoja wa hao marafiki zangu ni Christian Mlelwa ambaye kwa sasa yupo Ludewa kijijini Mavanga; nilipotengeneza mashine ya kwanza, aliiona na kuipenda; ikabidi aninunulie vifaa vya kutengeneza nyingine na kunipa pesa ya ufundi; nikamwachia.”

Anaongeza: “Mashine ya tatu ipo maeneo ya Ilembuka katika Wilaya ya Wang’ingombe (mkoani Njombe) akiitumia Erick Mwakidika ambaye sasa ni mmiliki wa kiwanda cha kukamua mafuta.”

Mbunifu huyo anasema ili kukamilisha mashine moja, zinahitajika takriban Sh milioni tatu na kama vifaa vyote vinavyohitajika vinakuwapo, kazi hiyo huchukua muda wa takriban wiki tatu hadi nne (mwezi) kukamilika.

“Mashine kama hii, kwa saa 24 inaweza kukamua lita 600 za mafuta ya alizeti na kwa kuwa watu wengine ambao ni wateja huja kukamulia hapa, kwa kila kilogramu moja ya mbegu za alizeti inayokamuliwa, wanalipia sh 50 na hivyo, mashine kuwa chanzo cha mapato kwa kuhudumia wengine,” anasema mbunifu huyo anayetamani kupewa shahada ya heshima ya udaktari.

SHUKRANI

Anasema alipimiwa shamba lake la ekari moja katika eneo la Magoda ‘C’ kupitia Mkurabita na bado hajapata hati ya hakimiliki yake anayosisitiza kuisubiri kwa hamu maana manufaa yake anayaona kwa wengine.

Anasema kitendo cha Mkurabita kurasimisha ardhi, mashamba na makazi ya watu na kupata hati hizo zilizowawezesha kufufua na kukuza mitaji yao, kinamnufaisha hata yeye kwa kuwa kadiri wanavyonufaika wengi na kuanzisha miradi kama kilimo cha alizeti, ndivyo anavyonufaika kwa kupata wateja.

“Wanaponufaika wengine na sisi hapa tunanufaika kwa kupata wateja ndiyo maana tunashukuru Mkurabita maana wametufufua kimtaji na kiuchumi,” anasema Kaduma.

MWELEKEO

Kuhusu matarajio na malengo yake, anasema: “Sasa hivi nipo katika mchakato wa kutengeneza mtambo wa kutengeneza chakula cha ng’ombe katika mashine ambayo ukiweka vigunzi na kuchanganya baadhi ya virutubisho, unapata chakula cha mifugo.”

Chanzo: habarileo.co.tz