Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Duwasa yaagizwa kasi kutatua kero za wananchi

F37fc58dd84241baff32502f9ace8e10 Duwasa yaagizwa kasi kutatua kero za wananchi

Fri, 22 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (Duwasa) imetakiwa kuongeza kasi ya utatuzi wa kero za wananchi ili kuleta tija katika mamlaka hiyo.

Akizindua baraza la sita la wafanyakazi wa Duwasa jijini hapa juzi, Naibu Waziri wa Maji Maryprica Mahundi alisema kero nyingine zimekuwa zikisababishwa na baadhi ya watu ambao wanashindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamika kutokana na huduma wanazozipata hivyo kupitia baraza hilo wahakikishe wanafanya kazi ya kuzitatua kero hizo ili wananchi wafurahie uwepo wa mtandao wa maji.

“Ifike mahali iwe inatosha kusikia malalamiko hayo, na ukiangalia wakati mwingine ni baadhi ya watu wanafanya kazi kwa mazoea, lakini tunahitaji kuona kwamba tunakuwa wabunifu na kujenga mtandao wa maji kuwa bora zaidi,” alisema Mahundi.

Alisema kuna kila sababu ya Duwasa kuendelea kuujenga mtandao wa maji kwa kuwafikishia wananchi huduma za maji kwani wanauhitaji huo huku akisema wizara itaendelea kuiwezesha ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Hata hivyo alisema Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za kuhakikisha kunakuwepo na uondoshaji mkubwa wa maji taka katika jiji la Dodoma unaojumuisha ujenzi wa kilomita 250 za mabomba pamoja na mabwawa 16 yatakayojengwa katika eneo la Nzuguni.

Aidha alisema lengo ni kuifanya Dodoma kuwa na sura ya Makao Makuu ya nchi.

Alisema ili mradi huo ufanikiwe kwa malengo yaliyokusudiwa lazima wananchi wapatiwe elimu ya kutosha kwani ni wachache wanaofahamu kuwa wanaweza kuunganishiwa mfumo huo kutoka kwenye makazi yao hadi kupeleka maji taka kwenye mabwawa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka Profesa Faustine Bee alisema ili kukabiliana na changamoto ya upungufu Dodoma wanaishawishi Serikali na wadau wengine kuongeza kasi ya uwekezaji.

Profesa Bee alisema Duwasa peke yake haitaweza kuwekeza kwenye miradi mikubwa ili kutatua tatizo kubwa la ukosefu wa maji katika jiji la Dodoma.

Alisema wanaendelea kuboresha huduma ya maji ili kuinua uwezo wa maeneo waliyopewa kuyasimamia hususani, Mpwapwa, Bahi na Chamwino na Kongwa kwa lengo la kuifanya mamlaka kuwa bora ndani ya Bara la Afrika.

Chanzo: habarileo.co.tz