Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dodoma yaiburuza tena Dar makusanyo

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Baada ya taarifa ya ukusanyaji wa mapato mwaka 2017/18 kuonyesha kwamba Mkoa wa Dodoma uliongoza kukusanya asilimia 170 hadithi imeendelea kuwa ileile baada ya safari hii halmashauri ya manispaa yake kuzipiku nyingine zote zikiwamo za Mkoa wa Dar es Salaam.

Akitoa tathmini ya ukusanyaji huo wa mapato wa robo mwaka ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alisema Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekusanya Sh14.4 bilioni kati ya Sh68.6 bilioni sawa na asilimia 21 ikifuatiwa na Ilala iliyokusanya Sh11.2 bilioni kati ya Sh56 bilioni sawa na asilimia 20, huku Kinondoni ikikusanya Sh7 bilioni kati ya Sh32.7bilioni sawa na asilimia 21.

Temeke imekusanya Sh6.5 bilioni kati ya Sh32.3 bilioni sawa na asilimia 20 huku Arusha ikikusanya Sh4.1 bilioni kati ya Sh15.6 bilioni sawa na asilimia26.

Hata hivyo, Jafo alisema halmashauri ya Jiji la Arusha inaongoza kwa kukusanya vizuri kiasilimia kwani imekusanya Sh4.1 bilioni (asilimia 26) ya malengo iliyojiwekea ya Sh 15.6 bilioni katika mwaka wa Fedha 2018/19.

“Ieleweke wazi kuwa Jiji la Arusha ndio lililofanya vizuri kimakusanyo kwa mujibu wa asilimia lakini Jiji la Dodoma ndilo lililokusanya fedha nyingi zaidi kuliko halmashauri zote Tanzania,” alisema.

Jafo alisema halmashauri 76 zimefanya vizuri kwa kukusanya zaidi ya asilimi 20 huku akisema halmashauri zilizofanya vibaya katika makusanyo hayo ni 23 ambazo zimekusanya chini ya asilimia 10 ya makisio.

Alizitaja zilizofanya vibaya kuwa ni Masasi iliyokusanya asilimia 2, Nanyamba na Nanyumbu (3) Newala na Tandahimba (4), Songea, Madaba, Rorya na Morogoro (zote 5).

Jafo alisema katika kundi la halmashauri za manispaa zilizofanya vizuri zaidi ni Manispaa ya Musoma na halmashauri za mji zimeongozwa na Mbinga na upande wa halmashauri za wilaya zimeongozwa na Kisarawe.

Waziri Jafo aliwakumbusha viongozi wanaohusika kuwa ukusanyaji wa mapato ndio kigezo cha utendaji kazi wao hivyo kila mmoja ajitathmini kulingana na mapato ya halmashauri/mkoa wake.

Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19 halmashauri nchini zilipangiwa kukusanya Sh 735.6 bilioni kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani. Jafo Alisema hadi kufikia Septemba 30, halmashauri zilikusanya jumla ya Sh143.6 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 20 ya makisio ya mwaka.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2017/18 halmashuri zilipangiwa kukusanya Sh687.3 bilioni na hadi kufikia Septemba 30, 2017 zilikusanya Sh126.8 bilioni sawa asilimia 18 ya makisio.

“Kutokana na takwimu hizo inaonyesha kwamba halmashauri zimeongeza wingi wa mapato kwa kiasi cha Sh16.7 bilioni na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani umeongezeka kwa asilimia mbili,” alisema Jafo.

Simiyu yaongoza

Kwa upande wa mikoa, Simiyu imeongoza katika makusanyo ya mapato katika robo ya mwaka wa fedha 2018/19 huku Mkoa wa Dar es Salaam ukikosekana katika orodha ya mikoa 10 iliyofanya vyema katika ukusanyaji licha ya halmashauri zake mbili; Ilala na Kinondoni kufanya vyema kwenye makusanyo.

Oktoba 5 mwaka huu, Waziri Jafo alitangaza makusanyo ya halmashauri za miji, majiji, manispaa na wilaya kwa mwaka 2017/18 na kuitaja Simiyu kuwa miongoni mwa mikoa mitatu iliyokusanya kwa asilimia ndogo, huku Dar es Salaam ikikusanya Sh138.3bilioni kati ya malengo ya Sh191.7bilioni iliyoji-wekea.

Katika taarifa za ukusanyaji wa mapato mwaka 2017/18, mikoa iliyoongoza ilikuwa Dodoma iliyokusanya asilimia 170 ya malengo, ikifuatiwa na Geita (104) na Njombe (103).

Jana, Jafo alisema mikoa 10 iliyofanya vizuri katika makusanyo kwa kukusanya juu ya asilimia 20 ni Simiyu uliokusanya asilimia 29, Manyara (28), Lindi (28), Mara (24), Pwani (23), Arusha (23) Njombe (22), Dodoma (22), Mwanza (21) na Geita (21).

Iliyofanya vibaya ni Mtwara uliokusanya asilimia sita ya makisio yake, Kigoma (13) na Ruvuma (11).



Chanzo: mwananchi.co.tz