Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dodoma kujinasua hatari ya Ukimwi

Bade76b132c4263fba2a3a7465e686ae.png Dodoma kujinasua hatari ya Ukimwi

Fri, 4 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKOA wa Dodoma unatakiwa kuweka mkakati wa makusudi kuunasua kutoka kundi la mikoa yenye maambukizi makubwa ya virusi vya Ukimwi kutokana na kuongezeka kutoka asilimia 2.9 mwaka 2013/14 hadi asilimia tano katika mwaka 2019/2020.

Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi kimkoa yaliyofanyika jijini humo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Kessy Maduka alisema ipo haja kwa mkoa huo kuweka mikakati ya makusudi ili kuutoa katika kundi la mikoa yenye maambukizi makubwa ya virusi vya Ukimwi ilivyo sasa.

"Miaka iliyopita tulikuwa kwenye mikoa yenye maambukizi kidogo ya Ukimwi lakini sasa tupo kwenye mikoa hatarishi, hapa ni lazima tuweke mikakati ya kupambana nayo kwa pamoja, Dodoma kamwe haiwezi kukubali hali hii," alisema.

Maduka pia alitoa rai kwa kundi la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU) kutokata tamaa na kutopoteza matumaini, wanatakiwa kuendelea na mapambano na kusonga mbele katika mapambano dhidi ya maradhi hayo.

Akijibu maombi matatu yaliyotolewa wakati wa kusoma risala ya Waviu la uhaba wa mtaji, eneo la kufanyia biashara na kushirikishwa kwenye kutoa ushauri kwenye hospitali na vituo vya afya, aliahidi kuwasaidia.

"Ombi la kushirikishwa kwenye kutoa ushauri niwakaribishe ofisini kwa ajili ya kufanya mazungumzo na kuhusu eneo la biashara ombi hili nimelipokea na nitalifikisha kwa wanaohusika kwa hatua zaidi," alisema.

Maduka alisema takwimu za kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi, zimetokana na utafiti wa Tanzania Health Impact Survey (THIS) unaofanyika kwenye kaya kila baada ya miaka mitano. Utafiti huo umeonesha uwepo wa ongezeko la asilimia 2.1 na kundi la vijana ndilo lenye maambukizi mengi zaidi.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalaganya alisema, unyanyasaji wa kijinsia umesababisha maambukizi mapya ya virusi hivyo.

"Niwaombe vijana mjitambue ili mfikie malengo yenu, nina imani kila mmoja akitimiza jukumu lake tutaweza kutokomeza maambukizi haya," alisema.

Awali, Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Dodoma Abdul Ahmed alisema makisio ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na wanaojua hali zao kwa mkoa ni 55,133. Hadi kufikia Septemba mwaka huu watendaji walishawafikia watu 35,064 sawa na asilimia 71 bado asilimia 29 tu kuwafikia.

"Kati ya idadi hiyo ya watu tuliowafikia asilimia 99.5 tumewaunganisha katika huduma za tiba na matunzo ambapo kati yao asilimia 85 wamefanikiwa kufubaza virusi hivyo," alisema Ahmed.

Mratibu huyo alitaja baadhi ya changamoto zilizopo katika mapambano dhidi ya virusi hivyo kuwa ni uwepo wa unyanyapaa na idadi ndogo ya wanaume wanaojitokeza kupima afya zao.

Akisoma risala ya Waathirika wa Virusi vya Ukimwi, Anamary Oscar ambaye ni mjasiriamali wa kutengeneza batiki, alitoa ombi la eneo la kufanya ujasiriamali na kuwataka vijana kujiunga kwenye vikundi ili kopesheke.

Kaulimbiu ya Siku ya Ukimwi Duniani mwaka huu ilikuwa ‘Mshikamano wa Kimataifa Tuwajibike Pamoja’.

Chanzo: habarileo.co.tz