Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk. Shein aongoza maziko ya Prof. Luhanga

Luhanga (1) Dk. Shein aongoza maziko ya Prof. Luhanga

Wed, 22 Sep 2021 Chanzo: ippmedia.com

MKUU wa Chuo cha Mzumbe, Dk. Mohamed Ali Shein ameongoza waombolezaji katika maziko ya aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Matthew Luhanga, aliyezikwa kwenye makaburi ya Kwa Kondo, Tegeta jana jijini humo.

Prof. Luhanga alifariki dunia Jumatano iliyopita na maziko yake yalitanguliwa na ibada ya mazishi iliyofanyika Parokia ya Mt. Andrea Mtume, Bahari Beach.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, baadhi ya wakuu wastaafu wa chuo cha Mzumbe, UDSM na wasomi mbalimbali waliowahi kufanya naye kazi.

Katekista Robert Ikombe, alisema Prof. Luhanga alikuwa muumini wa kanisa hilo na alikuwa mwenye upendo na kujali.

“Nimebahatika kuongea naye mara nyingi, ulikuwa ukikaa naye hajivunii kwamba yeye ni msomi kwamba hawezi kuongea na mtu mwingine yeyote, alikuwa mtu anayepokea ushauri unaompa, alikuwa mtu wa watu,” alisema.

Katekista Ikombe aliwaasa waumini kuwa maisha ni mafupi na kuwataka wafanye kazi ya Mungu kwa kuishi anavyoelekeza kuwapenda na kuwatumikia wale ambao wamekabidhiwa.

“Prof. Luhanga alikuwa na mamlaka makubwa, lakini katika maisha yake bado aliweza kutumika kwa hali yoyote ile,” alisema.

Mercy Luhanga, alisema Prof. Luhanga ni baba yake mdogo na alimlea, alikuwa kiongozi anayejali muda na mchapa kazi ambaye pamoja na majukumu mbalimbali alikuwa anajali familia.

“Wengi walipenda kumuita mbishi, alipenda kusimamia jambo ambalo aliliamini liko sawa,” alisema.

Prof. Anagisye alisema yapo mengi ya kujifunza kutoka kwa Prof. Luhanga ambaye akiwa Makamu Mkuu wa Chuo cha UDSM alibeba mzigo kwa ajili ya maendeleo ya chuo, kiongozi, mtafiti, mwanataaluma na mwadilifu na mzalendo ambaye aligusa maisha ya Watanzania na wataaluma wengine duniani.

Alisema Prof. Luhanga alikuwa jabali la mageuzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika masuala ya taaluma, utafiti, miundombinu na chuo kwa ujumla pia, sehemu ya  msingi alioanzisha kwenye chuo hicho.

 

Mhadhiri Mwandamizi Masuala ya Mipango ya Elimu, Prof. Herme Mosha, alisema Prof. Luhanga alikuwa mtu wa kuthubutu hata itoke amri kutoka serikalini alikuwa haikubali hivi hivi bila kutafakari.

“Alikuwa mtu anayeweka muda, aliheshimu watu na kila mtu alimuheshimu, vijana wajifunze kupitia yeye,” alisema.

Prof. Luhanga aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe.

Chanzo: ippmedia.com