Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mchararazo awataka Watanzania kujenga utamaduni wa kusoma vitabu

Fri, 23 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (Bohumata) Dk Alli Mcharazo amesema uchumi imara wa nchi unajengwa na watu wenye maarifa, hivyo ameiomba Serikali kuendelea kuwa na programu nyingi kwa ajili ya kuhamasisha jamii kupenda kusoma.

Aidha amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kusoma vitabu ili waweze kujiongezea maarifa.

Amesema kujisomea kutawawezesha kujifunza kuhusu maendeleo yao na ya watu wa mataifa mengine katika nyanja mbalimbali.

Akizungumza katika uzinduzi wa Tamasha la Usomaji kwa niaba ya Kaimu ofisa elimu msingi Manispaa ya Kinondoni, Abdallah Mchia, leo Alhamisi Novemba 22, 2018 Dk Mcharazo amesema uchumi wa viwanda utajengwa na watu wenye maarifa yapatikanayo kwa njia ya kusoma.

Amesema takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa zinaonyesha katika nchi zinazoendelea zikiwemo za Kusini mwa Jangwa la Sahara, mtu mmoja pekee kati ya watano hana kabisa ujuzi wa kusoma na kuandika na robo tatu kati yao ni wanawake.

“Hii ni changamoto kwetu sote hivyo, hatuna budi kushirikiana kuhakikisha utamaduni wa kujisomea unaimarika katika ngazi zote,”amesema.

Tamasha hilo lililoandaliwa na Maktaba Kuu ya Taifa Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) umehusisha wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi.



Chanzo: mwananchi.co.tz