Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mashinji acharuka wazazi waliopiga marufuku watoto kula chakula shuleni

Mashinji Vicent Dk Mashinji acharuka wazazi waliopiga marufuku watoto kula chakula shuleni

Mon, 6 Feb 2023 Chanzo: Mwananchi

Imeelezwa kuwa imani za kishirikina ni moja ya sababu kwa Mkoa wa Mara kushindwa kutoa chakula cha machana kwenye shule za umma ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa afua za lishe.

Mwaka jana Mkoa wa Mara ulikuwa wa mwisho kwenye utekelezaji wa afua hizo baada ya shule nyingi za umma kushindwa kutoa chakula cha mchana shuleni sambamba na wakurugenzi wa halmashauri kushindwa kutenga bajeti ya Sh1,000 kwa kila mtoto kwaajili ya kuwezesha utekelezaji wa shughuli za lishe.

Akichangia kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe mjini hapa leo, Jumatatu Februari 6,2023, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dk Vicent Mashinji amesema kuwa moja ya viashiria vya utekelezaji wa afua za lishe ni pamoja na utoaji wa chakula cha mchana shuleni lakini suala hilo limekuwa gumu kutekelezwa kwasababu mbalimbali ikiwemo imani za kishirikina.

"Utaratibu wa kula pamoja ni mgumu kwa baadhi ya maeneo kwenye Mkoa wa Mara kama vile kule Rorya na baadhi ya maeneo wilayani Bunda na hii inatokana na imani iliyopo katika jamii hizo wakiamini kuwa wakila hadharani watalogwa na watakufa," amesema.

Ameongeza kuwa yapo baadhi ya maeneo watu wanashindwa kula hata misibani kutokana na imani hiyo, huku akisema kuwa wazazi wamefikia hatua ya kuwazuia watoto wao kula hadharani na kwamba kutokana na hali hiyo inakuwa ni vigumu kwa watoto kupata chakula shuleni.

"Sisi tumekaa na wazee wakasema wapo tayari kuchangia chakula shuleni lakini watoto wao siyo lazima wale shuleni, sasa niombe tuangalie namna ya kutekeleza sera hii ya lishe shuleni kulingana na mazingira ya eneo husika," amesema.

Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amewaagiza watendaji wa serikali kutekeleza maagizo ya serikali bila kuwa na visingizio ikiwemo agizo la kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi kwenye shule zote za umma.

"Haya kuna uchawi kwa hiyo tuwaache watoto wasipate chakula kisa watoto watalogwa hebu kila mmoja atimize wajibu wake," amesema.

Ameagiza kila shule kuhakikisha inakuwa na jiko kwa ajili ya kuanza mara moja utaratibu wa kutoa chukula shuleni ili kuwanusuru watoto ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakishindwa kufikia ndoto zao za elimu.

"Ni aibu tunakutana kwenye kikao cha tathmini chini ya uenyekiti wa Rais wetu halafu mimi Jenerali mzima nasimama eti mkoa wangu umekuwa wa mwisho, hii haikubaliki lazima tufanye jambo naagiza ujenzi wa majiko uanze mara moja kwenye shule zetu zote," amesema.

Chanzo: Mwananchi