Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Kijaji anusa harufu ya ufisadi ujenzi wa madarasa Kigoma

12002 PIC+KIJAJI TanzaniaWeb

Wed, 15 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ameiagiza kamati ya ulinzi na usalama wilayani Kigoma kufanya uchunguzi na kuchukua hatua baada ya kubaini harufu ya ufisadi katika ujenzi wa madarasa tisa ya Shule ya Msingi Kigoma yanayojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kwa gharama ya Sh200 milioni.

Dk Kijaji alitoa maelekezo hayo jana baada ya kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Dk John Tlatlaa kueleza kwamba mradi huo unahusisha ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa na vyoo vyenye matundu 12, wakati mkataba ulioingiwa kati ya manispaa na mkandarasi unaonyesha yatajengwa madarasa tisa na vyoo vyenye matundu 12.

Baada ya mjadala kati yake na Dk Tlatlaa, naibu waziri alimwelekeza kaimu mkuu wa wilaya hiyo, Mwanamvua Mrindoko kuchukua hatua za uchunguzi.

Pia, Dk Kijaji alibainisha kutoridhika kwake na gharama za ujenzi wa darasa moja kwa Sh17 milioni na kwamba kiwango cha Sh200 milioni kilichotolewa na Japan kutekeleza mradi huo kingeweza kujenga madarasa hata 20.

Awali, akitoa maelezo yake kuhusu ujenzi wa mradi huo unaojengwa na kampuni ya Juve Construction and General Trading ya mjini Kigoma, Dk Tlatlaa alisema Serikali ya Japan ilitoa masharti ya majengo hayo kujengwa na mkandarasi badala ya kutumia nguvukazi.

“Baada ya Japan kutuma fedha hizo na kuingia kwenye akaunti ya manispaa tulimwita mkandarasi na kumweleza kuwa kutokana na wingi wa fedha hizo, atalazimika kuongeza darasa moja zaidi,” alijitetea kaimu mkurugenzi huyo.

Alisema kutokana na sababu hizo majengo mapya yatawekewa nguzo ndiyo maana gharama zake zipo juu.

Hata hivyo, maelezo hayo hayakumridhisha Dk Kijaji na kuamuru uchunguzi wa kina ufanyike.

Chanzo: mwananchi.co.tz