Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jiinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima amesema amefurahishwa na Taasisi ya Karibu Tanzania Organization (KTO) kwa jitihada inazofanya za kuzalisha wataalamu wa malezi na makuzi ya awali ya watoto.
Dk Gwajima amebainisha hayo leo Jumatatu Desemba 13, 2021 wakati wa uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) mabao umefanyika jijini Dodoma.
Amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ya mfano katika taasisi nyingi zilizoshiriki kwenye uzinduzi wa programu jumuishi ya malezi ya mtoto kwa kutoa wataalamu wa kusimamia mpango huo.
Amesema kutoa huduma bila kuwa na malengo ya mbele haitakuwa nzuri lakini kuzalisha wataalamu ni jambo la msingi kwa mustakabali wa siku za mbeleni.
"Kufundisha wataalamu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ni jambo nzuri sana, nimelipenda, naamini kuwa wanaofundishwa watakuwa chachu ya kuzalisha watu wenye uelewa na faida kwa nchi," amesema Dk Gwajima.
Ofisa mawasiliano na mahusiano wa KTO, Symphrose Makungu amesema kwa kutambua umuhimu wa malezi ya mtoto, taasisi yao ilianza kutoa elimu katika vyuo 10 nchini ambako wanaendelea kuzalisha watoa elimu vijijini.
Makungu amesema wanatoa elimu hiyo katika vyuo vya Maendeleo ya Jamii (FDs) vilivyoko katika mikoa 8 ya Tanzania Bara ambako hadi sasa washiriki 125 wamefuzu hivyo wanaendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk John Jingu amesema mpango huo ulianza tangu 2019 na ni wa kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kabla ya uzinduzi, kulikuwa na mafunzo ya mpango huo yaliyowashirikisha waandishi wa habari za watoto, Waganga wakuu wa mikoa na Maofisa wa elimu kutoka mikoa mbalimbali nchini.