Arusha. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amewataka vijana wa jamii ya Kimasai kuiunganisha jamii yao kwa kudumisha mila na desturi .
Dk Bashiru amesema hayo leo Jumamosi Julai 6, 2019 katika sherehe ya uzinduzi wa boma la Eunoto katika Kijiji cha Mti mmoja wilayani Monduli huku pia akitaka kudumisha nidhamu ili kupata maendeleo.
Amesema ili kutetea maslahi ya jamii ya wafugaji, Serikali pia inapaswa kuweka ulinzi katika maeneo ya malisho ya mifugo yao yasivamiwe.
Hata hivyo, amewashukuru Rais John Magufuli na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa kutangaza undugu kati ya Kenya na kuwataka wananchi wake wafanye biashara kwa amani.
Mkuu wa viongozi wa Mila ya Kimasai, (Laigwanani) Lekisongo Meijo amesema Eunoto ni sherehe ya kimila ambayo inasimika viongozi wa vijana wa kimila wa jamii hiyo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoani Arusha, Loota Erasto Sanare ameiomba Serikali iisaidie jamii ya wafugaji kwa kuwapatia chakula kwa bei ya chini kwa sababu si wafugaji wote wanaojishughulisha na kilimo.
Pia Soma
- Sh1.5 bilioni kujenga chuo cha Veta Wilayani Kwimba
- Viongozi wawili Chadema wadaiwa watekwa
- Makubaliano ya Rais Magufuli, Kenyatta haya hapa