Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diwani ataka kasma kuongezwa shule ya Msingi Mlowa

1c9c37bfe2f7aa18b1609717d8846a84 Diwani ataka kasma kuongezwa shule ya Msingi Mlowa

Tue, 23 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

HALMASHAURI ya Itigi wilayani Manyoni mkoani hapa imetakiwa kuiangalia kwa jicho la pekee Shule ya Msingi Mchanganyiko Mlowa iliyopo mjini Itigi kutokana na shule hiyo kuchukua wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Mwito huo ulitolewa na Diwani wa Viti maalumu tarafa ya Itigi, Amina Msita wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22.

"Kabla ya kupitisha bajeti hii naomba kutoa angalizo juu ya Shule ya Msingi mchanganyiko Mlowa yenye walemavu zaidi ya 40. Kuna haja ya kuongeza bajeti kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya majengo rafiki kwa kundi hili" alisema na kuongeza:

“Baadhi ya wanafunzi waliopo wanaishi kwa ndugu, jamaa au kwa walimu wanaojitolea kuishi nao kutokana na kwamba wanatoka mbali, takribani kilomita 200 kutoka hapa. Ipo haja ya shule hiyo kuongezewa madarasa, kujengewa mabweni, jiko na bwalo la chakula ili kuwapunguzia adha wanafunzi hawa wenye mahitaji maalumu".

Akiunga mkono hoja hiyo, Diwani wa Kata ya Itigi, Ally Minja alisema suala la uwekezaji wa kudumu wa miundombinu ya majengo katika Shule ya Mchanganyiko Mlowa ni muhimu.

"Hii adha ya walemavu haiwahusu watoto wanaotoka mbali tu lakini hata wazazi walio karibu na shule bado wana kazi ya kumpeleka shule na kumrudisha nyumbani mwanafunzi mwenye ulemavu kwa kuwa hawezi kwenda shule na kurudi nyumbani peke yake" alieleza.

Ofisa Elimu ya Msingi wa halmashauri hiyo, Doreen Lutahanamilwa alisema mwelekeo wa serikali ni kuhakikisha kila mtoto anapatiwa elimu, bila kujali hali yake ya maumbile; hivyo kila halmashauri imeagizwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule waandikishwe.

Kikao hicho maalumu cha baraza la madiwani kilipitisha jumla ya Sh bilioni 22.75 ikiwa ni bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Chanzo: habarileo.co.tz