Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diwani aamsha hasira ya Halmashauri Jiji la Mbeya

Dcwilaya.png Diwani aamsha hasira ya Halmashauri Jiji la Mbeya

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, John Nchimbi, ametoa siku 30 kwa taasisi zote za Serikali kulipa malimbikizo ya ada za uzalishaji taka katika Kata ya Mbalizi road, jijini humo, vinginevyo hatua za kisheria kuchuliwa.

Hatua hiyo imefikia baada ya Diwani wa kata hiyo, Adamu Simbaya kuwasilisha hoja kwenye kikao cha Baraza la Madiwani robo ya kwanza, kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya jiji hilo, akitaka kusitishiwa huduma kwa taasisi ambazo zimeshindwa kulipia huduma hiyo kwa miaka sita.

“Mkurugenzi, Kata ya Mbalizi road tunashindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa ada za taka kutokana na taasisi za Serikali...kushindwa kulipa ada za uzalishaji wa taka,” amesema.

Amesema kufuatia changamoto hiyo ameomba kupata mwongozo wa kuwasitishia huduma za uondoshwaji wa taka mpaka hapo watakapolipa malimbikizo hayo kwani kitendo hicho kinakwamisha ukusanyaji wa mapato.

Amefafanua kuwa kwa upande wa mamlaka ya maji pekee wana deni la zaidi ya Sh7 milioni licha ya kufuatilia lakini hakuna majibu ya kuridhisha ya kulipa malimbikizo hayo jambo ambalo linawapa wakati mgumu katika makusanyo ya ada za taka.

Kufuatia hoja hiyo, Nchimbi amesema halimashauri hiyo itaziandikia taasisi hizo barua, ambayo itakuwa ni notisi ya siku 30, ikizitaka kufanya malipo ya malimbikizo ya ada hizo, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa.

“Inasikitisha sana taasisi za Serikali kushindwa kulipia malipo ya ada za taka kimsingi ntawasilisha barua, kwani...sisi tukihitaji huduma, huwa tunawalipa sasa inakuwaje wao hawalipi? Amehoji Mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake Naibu Meya wa Jiji la Mbeya, Kefasi Mwasote ameunga mkono hatua iliyotolewa na Mkurugenzi huyo huku akisema uchelewashwaji huo, unazorotesha makusanyo na mapato ya jiji hilo.

Mkazi wa Mtaa wa Mwasyoge katika kata hiyo, Sarah Brayson, ameomba halmashauri kuweka msisitizo kwa taasisi hizo kulipa ili kuboreshewa kwani wamekuwa wakisabisha uchafuzi wa mazingira kutokana na kutumia vijana kumwaga taka maeneo yasiyo rasmi.

Mwananchi ilipomtafuta Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mkoa, Neema Stanton kuzungumzia madai ya Sh7 milioni za ada ya taka, simu yake iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe wa meseji, haukujibiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live