Diwani wa Kata ya Ruvu Remit, mkoani Manyara, Yohana Maitei (Kadogoo) kupitia CCM, amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Simanjiro kwa kosa la kushambulia gari la CCM kwa mawe, akishirikiana na watu tisa.
Washtakiwa hao 10 wamesomewa shtaka hilo la kushambulia gari hilo mali ya CCM, wakati likiwa na wasimamizi wa CCM wa uchaguzi wa marudio ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Lerumo.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mosses Hamilton akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya, Charles Uiso amesema Maitei (45) amefanya kosa hilo akishirikiana na watu tisa.
Mwendesha mashataka Hamilton amesema katika kesi hiyo washtakiwa hao 10 wanadaiwa kufanya kosa hilo Februari 23 wakiwa kwenye Kijiji cha Lerumo, Kata ya Ruvu Remit.
Amewataja washtakiwa wengine ni Williams Yohana (36), Alamayani Kalusu (41), Petro Parkishu (45), Lekiton Olonyokie (65), John Abraham (42), Yohana Pakasi (53), Stive Sasin (69) Stephen Magirinai (69) na Alamayani Ngaisungui (70).
Amedai kuwa watuhumiwa hao waliharibu kwa shambulia gari aina ya Land Cruser mali ya CCM kwa kulipiga mawe na kusababisha uharibu uliogharimu kiasi cha Sh720,000.
Ametaja maeneo ambayo washtakiwa hao walishambulia gari hilo ni kioo cha mbele, na vioo vya pembeni ila hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa kwenye tukio hilo.
Hata hivyo, washtakiwa hao 10 walikana shtaka hilo na hakimu Uiso ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 14, 2023 itakoposomwa maelezo ya awali mahakamani hapo.