Dar/Mtwara. Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa wito kwa wakazi wa jiji hilo kusherekea kwa amani Sikukuu ya Pasaka huku ikionya wale wote watakaotaka kuvuruga amani watashughulikiwa.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Aprili 19, 2019 na Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu kuimarisha usalama katika Sikukuu ya Pasaka.
Mambosasa amesema jeshi la polisi limejipanga vizuri kuimarisha misako na doria ili kuhakikisha wahuni, vibaka, wezi na watu ambao hawataki watu wakae kwa usalama na utulivu kwenye kipindi cha sikukuu wanadhibitiwa kabla ya kuleta shida.
Amebainisha watakuwa na doria za miguu ambapo askari watatembea katika mitaa mbalimbali, pikipiki, mbwa, farasi, magari na helikopta ili kuhakikisha maeneo yote yanafikiwa.
Sambamba na hilo, amesema watashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha sherehe za Pasaka zinasherehekewa kwa amani na hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vinafanyika na endapo vitajitokeza vinadhibitiwa kwa haraka.
Ameongeza doria zitaimarishwa kwenye maeneo yote, yakiwemo ya nyumba za ibada, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Related Content
- Askofu awataka Wakristo kuwa na roho ya kusamehe
- Meneja mradi wa maji Chato akamatwa kwa agizo la Mbarawa
- VIDEO: Mwendokasi yaichana katikati gari ndogo, dereva afariki papo hapo
Kuhusu wamiliki wa kumbi za starehe wametakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa kumbi hizo kwa kuomba vibali vya kuendesha disko toto na hadi mchana alikuwa hajapokea kibali chochote cha kuomba kuendesha disko toto ili waweze kukagua kumbi hizo kama zipo salama hivyo amepiga marufuku disko toto kufanyika katika kumbi zote za Dar es Salaam.
Amewatahadharisha wale wote watakaokuwa wanaendesha vyombo vya moto kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani. Madereva wa magari kuepuka kujaza watu kupita kiasi.
Madereva wa pikipiki kuepuka kubeba mishikaki, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi ikiwamo pombe na endapo wakifanya hivyo wakikamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.
Kamanda Mambosasa amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu kwani jukumu la kuzuia uhalifu ni la kila mmoja.
Polisi Mtwara
Polisi mkoani Mtwara wamepiga marufuku disko toto kutokana na baadhi ya waandaaji kuwa na tamaa na kuwajaza watoto kupita kiasi katika kumbi.
Pia, wazazi na walezi wametakiwa kutowaruhusu watoto wao kwenda katika maeneo ya fukwe peke yao bila ya uangalizi wa mtu mzima atakayewaongoza.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa April 19, 2019 Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Blasius Chatanda amesema hatopenda kuona watoto wanapoteza maisha kama ilivyokuwa katika Sikukuu ya Krismasi mwaka 2018 ambapo wanafunzi wawili walifariki wakiogelea.
“Sote ni mashahidi Desemba watoto wawili walipoteza maisha wakiogelea kile tusingependa kijirudie, lakini wanapotoka wasiache nyumba wazi lazima wahakikishe kuna mtu mmoja anabaki kwa sababu wanapotoka vibaka na wao wanaweza kupata fursa,” amesema Chatanda.
Wakati huo huo Chatanda pia amewatahadharisha wanaokunywa na kulewa na kuwakumbusha kuwa wasingependa sikukuu hii iondoke na maisha ya watu na wanaotaka kustarehe waegeshe vyombo vya usafiri au kutafuta dereva ikiwa ni pamoja na kuvaa helmeti kwa waendesha bodaboda.
Mwendesha bodaboda mjini Mtwara, Salum Issa amesema baadhi ya abiria wamekuwa wakigoma kuvaa helmeti kwa madai ya kuwa zinatumika na watu wengi.
Amesema kutokana na hali hiyo wamekuwa wakilazimika kuwabeba hivyo hivyo ili wasikose fedha.
Dereva mwingine Said Nandope amesema kutokana na baadhi ya abiria kutovaa helmeti wamekuwa wakiwapatia na kuzishika mikononi wenyewe ili wanapokamatwa na polisi wa usalama barabarani waweze kujitetea.