Dismas Mrema (43), dereva wa gari la abiria aina ya Noah lililogongana na lori aina ya Scania na kuua watu watano na kuwaacha majeruhi wanne, amesimulia namna alivyopambana kuokoa maisha ya abiria tisa aliokuwa nao garini ajali hiyo ikitokea.
Ajali hiyo iliyotokea juzi jioni katika Barabara ya Mwika kwenda Himo katika eneo la CocaCola Riata wilayani Moshi baada ya breki za lori kutofanya kazi hivyo kuigonga nyuma kisha kuiburuza Noah hiyo umbali wa mita 374.
Mpaka sasa mwili mmoja tu umetambuliwa na ndugu na mingine imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Faraja huku baadhi ya majeruhi wakihamishiwa Hospitali za KCMC na Hospitali ya Mtakatifu Joseph iliyopo Moshi.
Akizungumza jana, dereva huyo ambaye amelazwa katika Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, alisema kutokana na lori hilo kuwa na spidi kali alishindwa kulikwepa.
Katika taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Scania kushindwa kulimudu gari hilo kwenye mteremko mkali. Dereva huyo aitwaye Elias Uledi alisema anashikiliwa kwa mahojiano na hatua zaidi za kisheria.
Dereva wa Noah afunguka
Akizungumzia ajali hiyo, dereva wa Noah, Mrema alisema dakika chache kabla ajali haijatokea, wakati anateremka kutoka Mwika katika Barabara ya Himo nyuma yake aliona kichwa cha gari kikishuka kwa mwendo mkali.
Alisema alijaribu kujihami kwa kulikimbiza gari lake ili kujinusuru na ajali lakini hakufanikiwa kwani hakukuwa na sehemu mbadala ya kuchepukia hivyo gari hilo ambalo lilikuwa nyuma yake lilimgonga na kuiburuza Noah hiyo kwenda kwenye mti uliokuwa pembeni ya barabara.
“Nilikuwa natoka Rombo kuja Moshi mjini na gari hilo la maji nililipita Mwika, lilikuwa linashuka taratibu lakini nilipofika huku chini nikaona kichwa cha gari kinanikimbilia nyuma na mwendo wake ulikuwa mkali sana. Nilijihami kwa kukimbia ila sikupata pa kukimbilia (kutokea) maana njia ni nyembamba na pembeni hakuna pa kuchepukia hivyo lori lile likanigonga kwa nyuma na kuniburuza hadi kwenye mti nje ya barabara,” alisema.
Muda mfupi baada ya ajali hiyo kutokea, alisema walilijikuta wamelala chini ya trela la maji huku baadhi yao wakiwa wamepoteza maisha.
“Bahati mbaya abiria watano walifariki palepale, wanne ni majeruhi na mmoja hakudhurika kabisa. Namshukuru Mungu naendelea vizuri, kwa sasa nasikia maumivu kwenye bega moja na mbavu nasubiri majibu ya x-ray,” alisema Dereva Mrema.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema kwa sasa wanamshikilia dereva wa lori, Elias Uledi kutokana na uzembe uliosababisha kupoteza maisha ya watu watano na kujeruhi wanne.
“Tunamshikilia dereva wa gari aina ya Scania lenye namba za usajili T303 AHD yenye tela namba T728 CWZ lililokuwa limebeba maji ya kunywa tani 30 lililoigonga Noah yenye namba T609 BGF na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi wanne,” alisema.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi Msaidizi wa Hospitali ya Faraja, Dk Doreen Massawe alisema walipokea miili ya watu watano na majeruhi wanne akiwamo majeruhi mmoja alivunjika nyonga ambaye amehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa matibabu zaidi.
“Majeruhi wawili ambao bado wamelazwa hapa ni dereva wa Noah ambaye alipata michubuko kwenye mapaja na mkono wake umeumia kidogo, yeye anaendelea na matibabu na mwingine ambaye ni kijana mdogo nyonga ilisogea na tayari tumeirudisha na anaendelea na matibabu ya mwisho hali yake inaendekea vizuri,” alisema Dk Doreen.