Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dawasa: Siyo lazima kulipia ili kuunganishiwa maji

31518 Dawasopic DAWASA

Fri, 14 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka (Dawasa), Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mwananchi anaweza kuunganishiwa huduma ya maji kwa mkopo na akalipa baadaye kwa makubaliano maalumu.

Luhemeja amesema hayo leo Desemba 13 wakati akielezea mafanikio ya siku 100 tangu kuunganishwa kwa Dawasa na Dawasco, Septemba 9 mwaka huu.

Amesema Dawasa imefanikiwa kutekeleza miradi yote saba ndani ya siku 100 kama alivyoahidi na kwamba wananchi wajitokeze kuunganishiwa huduma ya maji kwenye makazi yao.

"Mwananchi akitaka kuunganishiwa maji asilazimishwe kulipia, huduma hii inatolewa kwa mkopo wa miezi mpaka mwaka mmoja. Tunataka watu wengi wapate maji," amesema Luhemeja.

Amesema miradi ya ujenzi wa matenki ya maji katika maeneo ya Salasala, Wazo, Changanyikeni, Bunju na Bagamoyo imekamilika, hivyo wananchi hao watapata maji ya uhakika.

Mtendaji huyo amesema changamoto kubwa aliyokumbana nayo ni uhaba wa fedha za kukamilisha miradi hiyo, hata hivyo amesema Dawasa haina mpango wa kuongeza bei za maji kwa sasa.

"Katika uongozi wangu, Dawasa haitaongeza bei za maji, tunachofanya ni kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanaunganishiwa maji ili mapato yatakayopatikana yarudi kuhudumia wengine," amesema Luhemeja.



Chanzo: mwananchi.co.tz