Morogoro. Kukatika kwa Daraja la Kiyegeya wilayani Kilosa kumesababisha uhamisho wa kaimu meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoa wa Morogoro, Godfrey Andalwisye.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliagiza kurudishwa makao makuu kwa meneja huyo jana kwa madai ya kushindwa kusimamia na kufanya ukaguzi wa miundombinu hasa kwa kipindi hiki cha mvua.
Majaliwa alitembelea eneo hilo kujionea ujenzi unavyoendelea baada ya kuharibika Jumatatu kufuatia mvua mkubwa.
Alisema mkoa wa Morogoro una jumla ya wahandisi 12 na ameshangazwa kwa kutofanyika ukaguzi wa barabara na madaraja kwani wangeweza kugundua tatizo la daraja hilo mapema.
Alisema kwa kutofanya hivyo, inaonekana namna walivyofanya uzembe na kusababisha madhara makubwa kwa nchi.
“Tanroads mna bajeti ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na mna wataalamu wa kutosha, huu ni uzembe kwa kutokagua na kuangalia vipenyo kwenye madaraja na katika kipindi cha mvua kama hiki kunakuwa na takataka zinazoleta madhara kwa madaraja,” alisema.
Habari zinazohusiana na hii
- Ujenzi wa daraja lililokatika Moro-Dodoma waanza
- Daraja lasombwa na maji Morogoro, mamia ya abiria wakwama
- VIDEO: Waziri asema daraja lililokatika kukamilika leo
- Abiria wachache wasitisha safari za mabasi Dodoma kuelekea Morogoro, Dar es Salaam
Majaliwa alieleza kuona ni aibu kwa barabara hiyo inayotumiwa na mataifa mengi kushindikana kupitika.
“Jambo hili linaweza kusababisha hata matatizo ya kiafya kutokana kuwepo msongamano mkubwa. Kunaweza kutokea magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, corona na magonjwa mengine,” alieleza Majaliwa.
Waziri Mkuu alisema kutokana na hali hiyo ameagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na wataalamu wa barabara kutoka Morogoro na Dodoma kufika eneo kuangalia uwezekano wa kupata kwa barabara mbadala wakati daraja hilo likiendelea kukabaratiwa.
Majaliwa alilitaka jeshi kuweka madaraja ya chuma ya muda ambayo yataweza kuhimili kupitisha magari makubwa.
Akizungumza na wasafiri na wananchi katika eneo hilo, Majaliwa amewatoa hofu kuwa wataweza kutumia daraja hilo wakati wowote pindi litakapotengamaa.
Pia alisema Serikali inafanya kila jitihada za kuhakikisha huduma hiyo inarejea mara moja ili wasafiri waweze kuendelea na safari zao kama kawaida.
Waziri Mkuu Serikali inaelewa umuhimu wa barabara hiyo kwani inategemewa na nchi nyingi za ukanda wa maziwa makuu.
Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alimuahidi Majaliwa kuwa watahakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili huduma ziweze kurejea.
Alisema wameongeza kampuni saidizi kwa ajili ya kuongeza nguvu kuhakikisha daraja hilo linakamilika mara moja.
Akizungumzia suala hilo, abiria Mohamed Issa anayeelekea wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma alisema tangu jana wapo katika eneo hilo baada ya kuahidiwa wangepelekwa kwenye basi jingine katika upande wa pili.
“Tulipita Msamvu na tulipofika hapa mizani tukasimamishwa na kuelezwa haturuhusiwi kwenda mpaka daraja litakapotengemaa,” alieleza Issa.
Issa anasema wamekuwa na wakati mgumu kwenye eneo hilo kwani sahani ya chakula cha kawaida waliyokuwa wananunua Sh2,000 hadi Sh2,500 kwa sasa wanauziwa Sh3,500 hadi Sh4,000 au Sh4,500 huku vinywaji baridi vikiwa Sh1,000 hadi 1,500 kutoka Sh500 na Sh700.
Abiria mwingine Jonas Mdabi alisema kumekuwa na shida ya watu kuoga na kupata huduma ya choo.
Utingo wa lori mojawapo lililokwama linalokwenda Rwandam Abeid Amani alisema kwa siku tatu wamekuwa mkoani Morogoro wakisubiri kukamilika kwa daraja.