Baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Mpanda wamesema kukamilika daraja la Tulieni linalounganisha mawasiliano kati ya Mpanda na Nsimbo limekuwa fursa katika shughuli za maendeleo.
Wamesema kukosekena kwa daraja hilo kwa muda mrefu kuliwasababishia adha wakati wa masika huku wakitumia gharama kuvushwa kwenda kutafuta huduma za kijamii.
Wakizungumza na Mwananchi leo Desemba 29, 2021 baadhi ya wananchi wa Mpanda wamesema hali hiyo iliwaathiri kiuchumi wakidai kuwa wanafunzi nao walikatisha masomo wakati wa masika.
Mkulima Dioniz Stephano amesema kabla ya kufanyiwa matengenezo daraja hilo linalounganisha barabara ya Mtapenda na Nsemlwa Mpanda wengi walikosa mahitaji muhimu ya kifamilia.
Amesema walikuwa wanakumbana na adha ya kuvuka eneo hilo kwenda kutafuta mahitaji huku akibainisha kuwa wakati mwingine iliwalazimu watu hao kutoa fedha ili kuvushwa kwa kubebwa mgongoni.
“Watu walikuwa wanavua nguo wanavuka, wengine wanarudi na biashara zao kichwani, wenye uwezo walikuwa wanalipa Sh1000 hadi Sh2000 wanavushwa wanabebwa mgongoni tulilalamika sana,”amesema Stephano akaongeza.
“Hii hali ilisababisha wanafunzi kurudi nyumbani walikuwa hawaendi shule, maeneo haya yalikuwa hayana umeme tulilala njaa kwakukosa sehemu ya kusaga tumefurahi limetengenezwa,”
Naye mfanyabiashara mbogamboga na matunda kutoka Mtapenda, Hellena James amesema kuwa walikuwa wanaathirika zaidi ni wanawake na watoto kuliko wanaume.
“Tunashukru Mungu hali ni nzuri sasa hivi, tulikuwa tunashindwa kuendesha biashara zetu, usafiri wa magari, bajaji na pikipiki zilikuwa hazipiti hapa,”amesema Hellena.
Ofisa Mtendaji wa mtaa wa Tulieni, Mwanamvua Chambala katika taarifa yake kwa Mbunge wa jimbo la Mpanda mjini Sebastian Kapufi wakati akikagua ujenzi wa daraja hilo amesema limegaharimu amesema daraji hilo limegharimu Sh125 milioni.
“Limejengwa kwa usimamizi wa Tarura kwa njia ya mkandarasi aliyeanza mwezi Mei 2021 na kukamilisha Augosti 2021 limeondoa adha kwa wananchi,”amesema Mwanamvua.
Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi akizungumza na baadhi ya wananchi wa eneo hilo amesema kuwa ukosefu wa daraja hilo kwa muda mrefu ulikuwa kikwazo kwa maendeleo hivyo kwa sasa kukamilika kwa daraja kumekuwa fursa.
“Lilininyima usingizi kutokana na malalamiko ya wananchi, nilimfuata Mtendaji Mkuu wa Tarura nikamuomba aninusuru, nifanyaje?” amesema Kapufi akaongeza.
“Aliniambia subiri niletee bajeti yote sikuamini lakini ametekeleza, kazi ya maendeleo ukubwa wake unaletwa na kusogeza huduma kwa wananchi naishukru sana serikali,”