Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daraja lakatika, laathiri usafirishaji Musoma - Mwanza

Picha Daraja Daraja lakatika, laathiri usafirishaji Musoma - Mwanza

Wed, 3 May 2023 Chanzo: mwanachidigital

Daraja la mto Nyamika Wilaya ya Butiama mkoani Mara limekatika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kutatiza shughuli za usafirishaji katika Barabara Kuu ya Musoma – Mwanza.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mara, Vedastus Maribe amesema daraja hilo limebomoka baada yam to huo kufurika hadi maji kupita juu kutokana na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia leo Mei 2, 2023.

"Tayari tumeanza matemgenezo dharura ambayo naamini yatakamilika ndani ya siku mbili au tatu kurejesha mawasiliano. Kwa sasa barabara hii imefungwa kwa muda na magari yote yanayoenda na kutoka Mwanza au Musoma yanatumia njia ya Butiama,” amesema Maribe

Kufungwa kwa barabara hiyo yenye magari mengi yanayotoka na kwenda mikoa mbalimbali nchini hadi nchi jirani ya Kenya kunaongeza muda na gharama za usafirishaji kwa sababu magari yote yanazungukia Butiama umbali wa takribani kilomita 30.

Akizungumzia hali ya miundombinu ya barabara mkoani Mara, Maribe amesema baadhi ya maeneo yameathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha akitaja mfano wa daraja la mto Tigite barabara ya Tarime –Mugumu lilifurika hadi maji kupita juu na kulazimisha magari kusubiri yapungue kabla ya kuendelea na safari.

“Daraja la Suguti pia kwenye barabara ya Musoma - Busekela kulikuwa na shida lakini magari yameanza kupita bila shida,” amesema Maribe huku akiwasihi watumiaji wa barabara mkoani humo kuwa makini na kuchukua tahadhari wanapoona maji yanapita juu ya barabara

Julius Wambura, mkazi wa kijiji cha Nyamika amesema waligundua kukatika kwa sehemu ya daraja asubuhi ya leo Mei 2, 2023 na kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji ambao nao umewasiliana na mamlaka zingine kutoa tahadhari kuzuia madhara ikiwemo ajali.

"Tunamshukuru Mungu hakuna madhara kwa binadamu maana magari yakiwemo mabasi ya kutoka mikoa mbalimbali yanatumia njia ya Butiama,” amesema Wambura

Chanzo: mwanachidigital