Kutokana na mvua kubwa zinazonyesha ukanda wa Morogoro na Selous, daraja la Mto Muhuwesi lililopo Wilaya ya Tunduru mkoani Songea limejaa maji hivyo kuchukua uamuzi wa kufunga barabara kuu ya Mangaka - Tunduru Mjini kwa muda.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro leo Februari 13, 2024 imebainisha eneo la barabara linalofungwa ni la mto lililopo kati ya kata za Muhuwesi na Majimaji.
“Magari yanayotokea Mbeya, Iringa, Songea na Mkoa wote wa Ruvuma kuelekea Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es Salaam yanapovuka Tunduru Mjini yapaki na kupumzika kusubiri hali iwe sawa Mto Muhuwesi. Magari hayo yanaweza pia kusimama/kupaki na kusubiria Sisi kwa Sisi au Muhuwesi kijijini,” imebainisha taarifa hiyo.
Pia, imebainisha magari yanayotokea Mkoa wa Lindi, Mtwara, Pwani na Dar Es Salaam kuja Tunduru, yanashauriwa kuegeshwa Nakapanya, Namiungo au Majimaji.
Kiongozi huyo amewataka madereva wasilazimishe kuvuka daraja hilo kwa sababu wataleta madhara na kuongeza kuwa vyombo vya usalama vimechukua tahadhari zote, visikilizwe.