Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daraja korofi barabara ya Arusha-Moshi kumaliza kero

 NBpa7gi.jpeg Daraja korofi barabara ya Arusha-Moshi kumaliza kero

Fri, 1 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Changamoto ya Daraja la Biriri kufurika maji wakati wa mvua na kukata mawasiliano ya barabara katika eneo la kwa Msomali, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, inatarajiwa kumalizika Oktoba mwaka huu, baada ya kukamilika kwa daraja kubwa linalojengwa katika eneo hilo.

Daraja hilo limekuwa na changamoto ya kufurika maji wakati mvua kubwa zinaponyesha na kukata mawasiliano ya Barabara Kuu ya Moshi-Arusha katika eneo la kwa Msomali, ambapo mwezi Aprili mwaka huu lilikata mawasiliano ya barabara hiyo kwa zaidi ya saa 4, baada ya maji kufurika juu ya daraja,hali ambayo pia ilihatarisha usalama wa watumiaji wa barabara hiyo.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa daraja hilo, Meneja Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Kilimanjaro, Motta Kyando amesema Serikali iliamua kubomoa daraja lililokuwepo na kujenga lingine kubwa ili kumaliza changamoto ya kukatika kwa mawasiliano ya barakara katika eneo hilo kipindi cha mvua.

Amesema mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika kabla ya Oktoba 18 mwaka huu, utagharimu Sh990 milioni hadi kukamilika na kwamba wanaamini kazi itakamilika kwa viwango na ubora uliokusudiwa.

"Mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, katika eneo hili tulipata mafuriko ambapo maji yalipita juu ya daraja. Hali hiyo ilisababisha tusimamishe shughuli zote za usafiri kwa zaidi ya saa nne hadi maji yalipopungua na baada ya changamoto hiyo. Tuliwasiliana na Tanroads makao makuu ili kuweza kutengeneza daraja kubwa ambalo linaweza kupitisha maji bila kuathiri watumiaji wa barabara hii, kwani lile lilikuwa dogo na tuliona kutokana na mabadiliko ya tabianchi, tunatakiwa kujenga daraja kubwa zaidi," amesema Kyando.

Amesema mpaka sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 35 na kimkataba wanatarajia kazi itaisha Oktoba 18 mwaka huu, lakini kutokana na taatifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) za uwepo wa mvua za el-nino, wamezungumza na mkandarasi kuongeza kasi ili kukamilisha mradi kabla ya Oktoba.

"Kutokana na taarifa tunazozipata kutoka TMA ni kwamba mwaka huu kuna uwezekano kukawa na mvua za El-nino hivyo tumewasiliana na mkandarasi ili aweze kuongeza kasi katika utekelezaji wa mradi huu na kukamilika kabla ya mwezi oktoba kwa sababu mvua hizo zinaweza kuanza kabla ya hapo na amekubali na kufanyia marekebisho programu yake ya kazi na tunaamini kazi itakamilika kabla ya msimu wa mvua kuanza."

Aidha amewataka wananchi kutoa ushirikiano wakati huu mradi unatekelezwa ikiwa ni pamoja na kufuata alama za barabarani zilizowekwa na maelekezo yanayotolewa ili eneo hilo liendelee kuwa salama

"Niombe wananchi watunze miundombinu ya barabara maana huwa kuna changamoto ya wizi wa vifaa na alama lakini pia wakati mwingine kuna uharibifu wa kuchimba mchanga, tuombe walitunze daraja ili lifanye kazi vizuri na lidumu kwa muda mrefu."

Meneja mradi kutoka Kampuni ya Rock Tronic ambao wanatekeleza mradi huo, Catherine Ritte amesema walianza mradi huo Juni 20, 2023 na kwamba kwa sasa wamefikia hatua ya kusuka vyuma na wanatekeleza mradi usiku na mchana ili kuukamilisha kabla ya msimu wa mvua kuanza.

"Kutokana na taarifa za uwepo wa mvua kubwa, tumeongeza juhudi za utekelezaji wa mradi na kwa sasa tunafanya kazi usiku na mchana lengo likiwa ni kumaliza kazi hii kabla ya mwezi oktoba, ili kuweza kuruhusu shughuli za usafirishaji katika barabara hii kabla mvua hazijaanza kunyesha," amesema.

Naye Pascal Vesto mkazi wa Bomang'ombe amesema ujenzi wa daraja hilo kutawezesha tatizo la maji kupita juu ya barabara kumalizika.

"Uwezo wa daraja lililokuwepo hapa ulikuwa mdogo na hivyo lilikuwa haliwezi kukidhi maji yaliyokuwa yakipita hapa hivyo mvua zikinyesha maji yalijaa juu ya daraja na barabara haikupitika kwa saa nne hadi tano lakini hili daraja linalojengwa sasa ni kubwa na inaonekana itakuwa ndiyo mwisho wa tatizo hilo," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live