Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daraja jipya Wami kunufaisha EAC

349b7ed64d1b789f37848dafef7853d0.png Daraja Wami

Tue, 21 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UJENZI wa Daraja jipya la Mto Wami uliopo Mkoani Pwani linatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) litakapokamilika.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi), Elias Kwandikwa alipozungumza na gazeti la Habarileo Afrika Mashariki kuhusu ujenzi wake unavyoendelea ambapo umefikia asilimia 50.

Alisema mataifa yanayotarajiwa kunufaika moja kwa moja kuiuchumi kutokana na daraja hilo ni Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Daraja hili litatumiwa na mataifa ya Afrika Mashariki kusafirisha abiria na mizigo yao kutoka na kuingia nchi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Kwandikwa.

Hii maana yake ni kuwa Tanzania itanufaika kwa asilimia kubwa kutokana na biashara ya mataifa mbalimbali itakayowezeshwa na kukamilika kwa daraja hilo ambapo mataifa mengine ya ukanda wa Kusini yatalitumia.

Mataifa ya Kusini mwa Afrika yanayotarajiwa kulitumia daraja hilo ni Msumbiji, Malawi na Zambia kusafirisha mizigo na usafiri wa abiria. Pia alisema wapo wafanyabiashara wa Tanzania watakaotumia biashara zao katika mataifa ya Afrika Mashariki. Hii ni ishara kuwa daraja hilo litakuwa kiungo muhimu cha biashara EAC.

Kwandikwa aliwataka wafanyabiashara nchini Tanzania kutumia fursa hiyo kupanua biashara zao pamoja na kujenga viwanda kwa sababu ya upatikanaji malighafi imeboreshwa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli.

“Hii ni fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Mashariki kuimarisha biashara zao ili kupata kipato na kuondoa umasikini,” alisema.

Kukamilika ujenzi wa daraja hilo la urefu wa mita 510 linalojengwa na kampuni ya ujenzi ya Power Construction Corporation kupitia mikoa ya Kaskazini na Afrika Mashariki litaongeza fursa nyingi za kiuchumi kwa Taifa kupitia usafiri na usafirishaji wa abiria na mazao.

Ujenzi wa daraja jipya la Wami ni mkakati wa Serikali wa kuondoa adha ya wasafirishaji kwa daraja hilo lililojengwa mwaka 1959 ambalo halikidhi mahitaji ya magari kwa sababu ni jembamba na lenye njia inayopitisha gari moja.

Chanzo: habarileo.co.tz