Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar yazizima kwa vilio

0d8ec51cb76d61139ac0e39bca649878 Dar yazizima kwa vilio

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VILIO vimetawala miongoni mwa wakazi wa Dar es Salaam waliojitokeza kwa wingi kuaga mwili wa Dk John Magufuli ulipopitishwa katika barabara mbalimbali kutoka Kanisa Katoliki la St Peter Oysterbay Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwenda Uwanja wa Uhuru kutoa fursa ya wananchi kumuaga.

Barabara kuanzia Oysterbay, Morocco, Kinondoni, Magomeni, Kigogo, Ilala, Karume na Keko, zilifurika watu waliokuwa wamesimama pembezoni wakipunga, kutandika nguo na wengine wakilia kwa sauti.

Dk Magufuli ambaye alifariki Machi 17, mwaka huu saa 12 jioni katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam kutokana na tatizo la umeme wa moyo, ibada ya kumwombea ilifanyika jana katika kanisa hilo la St Peter kabla ya kupelekwa Uwanja wa Uhuru ambako viongozi, watumishi na wananchi walitoa salamu zao za mwisho na kuaga.

Wakati msafara ukipita kwenda uwanjani, wakazi wa Dar es Salaam walifurika huku wengine wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kumtakia heri Magufuli katika safari yake hiyo ya mwisho.

Eneo la Morocco walishuhudiwa watu wakilia kwa sauti na wengine wakionekana kuishiwa nguvu. Wengi wao wakiwa na matawi ya miti, walipungia jeneza lililobeba mwili wa Dk Magufuli ishara ya kumuaga.

Gari lililobeba mwili likiwa wazi lilifunikwa kwa bendera ya Tanzania huku likitanguliwa na msafara wa magari na pikipiki kama zilizokuwa zikiongoza msafara wake wakati wa uhai wake.

Baada ya kufika Kinondoni Mkwajuni, umati mkubwa wa watu ulijitokeza barabarani huku wanawake wakipiga mayowe na wengine wakionekana kuanguka hali iliyowapa shida askari waliokuwa maeneo hayo.

Nyimbo za maombolezo, ‘Parapanda italia…’ na ‘Hayupo’ zilisikika miongoni mwa wananchi waliokuwa maeneo mbalimbali ambako msafara ulipita. “Umetuacha baba” ni miongoni mwa sentensi zilizosikika Magomeni Kanisani.

Shughuli mbalimbali zilisimamama. Daladala na mabasi ya mwendokasi katika eneo la Magomeni yaliegeshwa kando huku abiria wakipunga na wengine wakilia.

Katika maeneo ya Kigogo hadi Karume, walionekana watu wakitandika khanga, mitandio na mashati katikati ya barabara na kuruhusu magari ya msafara kuyakanyaga ikiwa ni ishara ya heshima kwa Dk Magufuli.

Umati wa wafanyabiashara wa Karume Machinga ulijitokeza ambako wengi wao walikuwa wakilia. Chang’ombe Vea baadhi ya watu walibeba mabango yaliyosomeka ‘Kwa heri mpendwa wetu Rais Magufuli,’ ‘Kwa heri Jemedari wetu’ na lingine ‘Tutakukumbuka rais wa wanyonge.’

Magari ya msafara yalipata shida kutokana na wingi wa watu waliokusanyika hadi barabarani kutaka kushuhudia jeneza hali iliyolazimu kuwapigia honi watu hao waliokuwa wakilia.

Msafara ulipofika Keko Bora, askari kutoka Kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walisindikiza msafara pembezoni mwa gari lililobeba mwili wa Dk Magufuli kwa mwendo wa mchakamchaka hadi ulipoingia katika Uwanja wa Uhuru saa 4.30 asubuhi kwa ajili ya ibada maalumu pamoja na kuaga viongozi na wananchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz