Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar waendelea kupuuza tahadhari za corona

00cf4861234b6f5884c13de345374436.jpeg Dar waendelea kupuuza tahadhari za corona

Sun, 8 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

LICHA ya wananchi kutakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona wimbi la tatu (Delta), baadhi katika jiji la Dar es Salaam wameendelea kupuuzia tahadhari hizo zinazosisitizwa na wataalamu wa afya na viongozi.

Uchunguzi uliofanywa na HabariLEO umebaini kuwa, agizo alilotoa Mkuu wa Mkoa huo, Amosi Makala kuwataka watu kutojazana kwenye vyombo vya usafiri na kuvaa barakoa limepuuzwa.

Katika vyombo vya usafiri vya umma na binafsi kwa siku kadhaa idadi kubwa ya abiria walishuhudiwa wakiwa hawajavaa barakoa.

Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa abiria Mbagala kwenda Mbezi, Swalehe Othaman alisema sababu ya kujazana kwenye vyombo vya usafiri ni uchache wa magari wa daladala huku idadi ya watu ikiwa ni kubwa.

“Tunajikuta hatuna la kufanya kwa sababu watu ni wengi na magari ni machache hivyo ukisema usubiri unachelewa kazini au hutaenda kabisa, ndio maana inatulazimu kubanana kwenye gari. Kwa mfano hapa Mbezi Mwisho unaona watu wengi wanasubiri gari likija ni kugombania kupata nafasi sasa kwa hali hii tunaweza kukaa ‘levo siti’ kweli wakati tunabanana tu hayatoshi.”

“Unatakiwa uwekwe mfumo na serikali wa usafiri Dar es Salaam bila ya kusababisha mateso mengine kwa watu wakiwemo wanafunzi,” alisema.

Mkazi wa Ubungo, Fadhila Msami alisema hali ya usafiri hairidhishi katika kipindi hiki cha wimbi la tatu la corona kutokana na idadi ya magari kuwa ile ile, hivyo agizo la levo siti ni gumu kutekelezwa.

“Tunatamani sana kujikinga na tusibanane katika daladala, lakini changamoto ni usafiri yaani hata ukiamka saa 11:00 alfajiri utakuta abiria ni wengi kituoni kwasababu asubuhi kila mtu anawahi kazini na kingine utakuta watu hata barakoa hawavai wanapanda tu, wataalamu wanatuambia tuvae barakoa kwenye mikusanyiko lakini wapo ambao hawazingatii,” alisema.

Said Maluwa, dereva wa magari yanayofanya safari zake Gerezani na Makumbusho alisema ni muhimu abiria kujikinga lakini ‘levo siti’ inaweza kuwa maumivu kwao na abiria.

Chanzo: www.habarileo.co.tz