Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar kupatiwa dampo la kisasa

DarEsSalaam Dar kupatiwa dampo la kisasa

Sat, 26 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Nchi Ofi si ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo amekiri Mkoa wa Dar es Salaam unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa dampo la kisasa na kusema serikali imetambua hilo na mpango wa kulijenga umeshaandaliwa.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati akizungumza kwenye kipindi cha Baragumu kinachorushwa hewani mubashara asubuhi na kituo kimoja cha habari nchini. Jafo alisema hali ya usafi kwa sasa katika Mkoa wa Dar es Salaam imeimarika tofauti na kipindi cha nyuma lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya taka kutokana na kukosekana kwa dampo la kisasa.

“Changamoto kubwa ya Dar es Salaam ni ukosefu wa dampo, hivi sasa mkoa mzima unategemea dampo la Pugu Kinyamwezi ambalo nalo ni la zamani na halijajengwa kisasa kuchakata taka,” alisema Jafo.

Alisema serikali imeliona hilo na kuamua kuanzisha mradi wa kujenga madampo katika maeneo tofauti nchini ambako majiji nane yatanufaika na mradi huo.

Alitaja baadhi ya maeneo ambayo madampo hayo ya kisasa yatajengwa ni Arusha, Moshi, Tanga, Dodoma na Mwanza na kusema hali ya sasa katika dampo la Pugu Kinyamwezi ni mbaya.

“Tunataka kutunza mazingira, nielekeze wakurugenzi wote nchini kwenye halmashauri wahakikishe zabuni wanazotoa kwa wakandarasi wa kuzoa taka waelekezwe jinsi ya kuratibu ili kusiwepo na uchafuzi wa mazingira,” alisema Jafo.

Alisema dampo zitakazojengwa za kisasa zitakuwa na maeneo yaliyojengwa mahususi kwa ajili ya taka zinazofanana ili kurahisisha uchakataji wake na pia zile zinawezwa kuchakatwa na kutoa malighafi zitumike kutengeneza bidhaa nyingine.

Jafo alisema baadhi ya viwanda vya kutengeneza vinywaji baridi nchini vimeanzisha viwanda vya kuchakata chupa za rangi za vinywaji vyao zilizotumika na hiyo ni hatua nzuri ya kutunza mazingira lakini pia kutoa fursa za ajira kwa wananchi.

Akizungumzia maagizo ya Waziri Jafo, Meneja wa Kanda ya Mashariki- Kusini wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Hamadi Kissiwa alisema wataendelea kukagua viwanda vyote kuhakikisha vinatekeleza agizo la kuchakata chupa za rangi za bidhaa zao zilizotumika.

“Tutahakikisha maagizo ya waziri tunayatekeleza kwa sisi NEMC kufuatilia viwanda ambavyo bado havijaanzisha uchakataji wa chupa za rangi watumiazo kufanya hivyo,” alisema Kissiwa.

Aidha, alisema baadhi ya upungufu uliobainika kiwandani hapo kama utiririshaji wa maji taka na mengine wamewapa maagizo kushughulikia kero hiyo ya kwamba maji hayo yameshafanyiwa uchakataji kuondoa madhara kwa wananchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live