Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar kupata maji ya uhakika ifikapo 2025

Maji Dar kupata maji ya uhakika ifikapo 2025

Sat, 18 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam. Changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi 450, 000 wa maeneo ya Kibamba, Segerea, Ukonga na Temeke, itapatiwa suluhu ifikapo mwaka 2025 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi Bangulo wenye thamani ya Sh42 bilioni.

Mradi huo unatekelezwa kwa muda wa miaka miwili kuanzia mwezi Oktoba 2023 hadi Oktoba 2025, na unafadhiliwa na fedha kutoka Benki ya Dunia na ukikamilika unatarajiwa kuzalisha lita za ujazo 23,333 kwa siku.

Mradi huo unaanzia Kibamba itakapofungwa pampu ya kusukuma maji kupelekwa hadi tanki la Bangulo lilopo Pugu, lenye uwezo wa kuchukua lita za maji 9000 milioni na kusambaza huduma hiyo katika meneo tajwa.

Hata hivyo Wabunge na madiwani wa maeneo hayo wanaupigia chapuo mradi huo kama kura ya turufu itakayowabeba katika Uchaguzi Mkuu ujao huku wakielekeza siasa za Mkoa wa Dar es Salaam kwa sasa ni maji na miundombinu ya barabara.

"Maswali kutoka kwa wananchi yamekuwa mengi kuhusu changamoto ya maji na kukamilika kwake wananchi watatulia na tutakuwa na nafasi kubwa ya kutetea nafasi zetu uchaguzi ujao," amesema Diwani wa Pugu Station, Shaban Mussa.

Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu amesema: “Wakati nachukua nafasi hii ua ubunge, upatikanaji wa huduma ya maji jimboni hapa ilikuwa ni chini ya asilimia 40; na kwa muda mrefu nimekuwa akiomba huduma hiyo.”

Mtemvu ameongeza kwa kusema: "Ndani ya kipindi cha miaka mitatu, mambo niliyoomba; leo yamekamilika, tukianza na tanki la maji Tegeta A, na kwenye Tangi la mshikamano na wananchi wanapata maji."

Akizungumza baada ya utiaji saini na kumkabidhi mkandarasi eneo kwa utekelezaji wa miundombinu ya usambazaji maji Kusini mwa Dar es Salaam, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewashukuru wabunge wa maeneo hayo kwakuwa wanafanya kazi kwa umoja katika kupigania maslahi ya wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam.

"Anayelala na mgonjwa anajua mhemo wa mgonjwa, wabunge wamekuwa mstari wa mbele na wakati mwingine wamekuwa wakorofi wamekuwa wakiuliza maswali bungeni na kuja ofisini kuja kushawishi kuhakikisha mradi huu unatekelezwa," amesema

Amesema hata wakati wanaenda kwenye bajeti ya serikali wabunge hao waliweka msimamo wakisema bajeti haipiti bila kuingizwa mradi huo kwa ajili ya wananchi wao.

"Mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) inafanya kazi kubwa ikipata mafua nchi nzima inapata chafya, wizara haitakuwa kikwazo katika kuhakikisha Wakazi wa Dar es Salaam wanapata maji safi na salama," amesema.

Amesema wananchi hao wamepata changamoto ya maji kwa muda mrefu hivyo mkandarasi wa mradi huo anapaswa kutekelezwa kwa wakati na kuacha visingizio kwani fedha zipo.

"Jukumu alilonalo ni kuweka nguvu kazi,kazi ifanyike na ukamilike kwa muda ulipangwa na wasimamizi wa mradi msichezee msimamieni mkandarasi kwa uaminifu na weledi mkubwa ukamilike na wananchi wapate maji," amesema Aweso

Kuunganishiwa maji kwa mkopo

Waziri Aweso amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Dawasa, Kiula Kingu kuwaunganishia huduma ya maji bure Wananchi na kisha wakatwe kidogokidogo.

"Maji hayana mbadala, maji si kama wali ukikosa utapata ugali, mtu anayekosa maji madhara yake ni makubwa niwaombe Dawasa, kuna watu wanaweza kulipa moja kwa moja kuunganishiwa maji lakini vipato tunatofautiana kwa kuwa serikali imetoa fedha kwa ajili ya miradi mikubwa anayeshindwa kulipa muunganishieni na mkateni kidogokidogo," amesema

Ameiomba Dawasa kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana kuwatumikia wananchi huku akieleza hakuna taasisi iliyopiga hatua kwa kufanya Majungu na hakuna taasisi iliyofanikiwa kwa uchimbi uchimbi.

"Hizi nafasi Mungu ndiye anapanga, Mungu akitaka iwe inakuwa mmekuwa watulivu katika kipindi chote ambacho Kaimu Mkurugenzi ameweza kufanya kazi nielekeze bodi ya Dawasa ilete pendekezo nani atakuwa mkurugenzi wa Dawasa na mimi Waziri wa maji nitaligusi jambo hili kwa haraka likamilike," amesema

Pia amesema vijana wa maeneo hayo lazima wanufaike na utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo huku akieleza itashangaza kuona mkandarasi anatoka na wafanyakazi maeneo mengine.

"Vijana watakao shiriki katika ujenzi huu niwaombe ukiaminika aminika,kuna wakati mkiaminiwa na kupewa dhamana mara unasikia ameiba kifaa fulani mnaziba milango kwa vijana wengine kuaminiwa na kupata kazi," amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Dawasa,Kiula Kingu amesema wana miradi mingine midogomidogo kama Kibamba ni eneo lenye miinuko mingi wametenga Sh500 milioni kwa ajili ya usambazaji wa huduma hiyo.

"Maeneo mengine ni machimbo,mpigi Magohe,Mbezi Makabe na Ukonga tumetenga Sh 200 milioni kuhudumia maeneo ya Bomba mbili,kivule na Pugu Station na sehemu zingine," amesema

Kingu amesema katika jimbo la Segerea, Dawasa imetenga Sh300 milioni ili kujenga vituo vya kusukuma maji kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo Vingungu, Stakishari na kaya zaidi ya 1000 zitanufaika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live