WAKAZI wa Dar es Salaam wameagizwa kuvaa barakoa kila wakati katika sehemu zenye mikusanyiko ya watu wengi ikiwemo kwenye vyombo vya usafi ri wa nchi kavu na majini.
Pia wametakiwa kuvaa wakiwa katika vituo vya usafiri huo, sokoni, mikutanoni na kwenye sherehe.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla wakati alipotembelea Halmashauri ya Manispaa Ubungo katika ziara zake anazofanya toka alipoteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Mkuu huyo wa mkoa pia ametaka barakoa zivaliwe kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, maofisini, baa, migahawa na darasani kwa wanafunzi wa vyuo.
Katika agizo hilo amewataka wakuu wa wilaya, wakuu wa taasisi za serikali na zisizo za serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia maelekezo hayo kikamilivu.
Makalla alisema hivi karibuni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitoa taarifa ya kuwepo kwa mlipuko wa wimbi la tatu la ugonjwa wa Covid-19 kwenye nchi za Afrika zikiwemo nchi jirani.
“Taarifa imetaja pia kuwa nchini kwetu kuna viashiria pia vya wimbi la tatu, kutokana na muingiliano mkubwa uliopo kati ya mkoa wetu na nchi jirani, mkoa wetu na mikoa mingineyo ndani ya nchi,”alisema.
Alisema kutokana na viashiria hivyo ni vema wananchi wa Dar es Salaam wakachukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi hayo kwa kunawa kwa maji tiririka mara kwa mara na kwa sabuni, kutosogeleana kwa karibu kwa kuweka umbali angalau mita moja au kupaka vipukusi.
“Kufunika midomo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya kwa kutumia kiwiko cha mkono au kitambaa safi,” alisema.
Maagizo mengine aliyoyatoa yanawahusu wasimamizi kwenye maeneo yenye msongamano kuhakikisha wanaweka ndoo na miundombinu mingineyo ya maji tiririka na sabuni katika maeneo yote ya taasisi mbalimbali , vituo vya vyombo vya usafiri wa majini na nchi kavu na maeneo yote yenye msongamano.
Vilevile aliwataka wananchi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya haraka wapatapo dalili za ugonjwa huo kama homa kali, mafua makali, kikohozi, uchovu mkali, kushindwa kupumua, kushindwa kunusa au kupoteza uwezo wa kuhisi ladha ya chakula.
Alisema mgonjwa anapowahi kufika katika kituo cha kutolea huduma za afya mapema matokeo ya tiba yanakuwa ni mazuri zaidi.
Aliwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi kwani huimarisha kinga ya mwili pamoja na kula mlo kamili.
Ashauri walindwe wale walioko kwenye hatari ya kupata madhara makali zaidi ya Covid- 19 wakiwemo wazee, wenye magonjwa sugu kama shinikizo la juu la damu, kisukari, figo, kifua kikuu na magonjwa ya moyo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume alisema maagizo hayo yamezingatia miongozo ya Shirika la Afya Dunia (WHO) pamoja na Wizara ya Afya.