Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar, Kilimanjaro zatia aibu tupu kwa utapiamlo

Wed, 20 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Taasisi ya Chakula na Lishe nchini (TFNC) imetaja mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro kuwa vinara wa utapiamlo uliozidi kiwango cha chini.

Mwakilishi wa mkurugenzi wa TFNC, Geofrey Chiduo alisema jana katika mkutano wa kutathmini hali ya lishe na mahali walipofikia katika mpango wa kwanza wa lishe wa Agosti 2018.

Mkutano huo uliwashirikisha wakuu wa mikoa, makatibu tawala mikoa, baadhi ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wadau wa lishe.

“Hata katika mikoa ambayo uzalishaji upo juu viwango vya utapiamlo vipo katika viwango vya juu sana. Jambo lingine tunaotekeleza mkataba huu tunatakiwa kufahamu kwamba hata sisi wa mjini hatuna tofauti na wa maeneo ya vijijini. Hakuna aliye salama,” alisema.

Chiduo alisema hivi sasa wanapambana na maadui wawili ambao ni utapiamlo wa hali duni ya ukosefu wa virutubisho, lakini kuna utapiamlo wa lishe uliopitiliza.

“Naomba nilitamke hili rasmi hapa kwa kuwa viongozi mpo kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro, suala la utapiamlo wa hali iliyozidi wao ndiyo vinara,” alisema Chiduo.

Related Content

Alisema hata katika mikoa ambayo uzalishaji chakula upo juu hali ya utapiamlo ipo juu pia na viwango katika mikoa vinatofautiana.

Akifungua mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi) Selemani Jafo, aliagiza halmashauri 31 ambazo zimeshindwa kutoa fedha za lishe kujieleza kwa wakuu wa mikoa ndani ya siku 14.

“Tatizo ni utoaji wa fedha zilizotengwa kwenye lishe. Eneo ambalo halifanyi vizuri tusitarajie kupata matokeo mazuri. Kuna halmashauri 31 wameshindwa kufanya hivyo na zingine 21 zimeshindwa kutimiza mikataba ambayo mlikubaliana,” alisema.

Jafo alisema Desemba 19, 2017 alisaini mikataba na wakuu wa mikoa kuhusu usimamizi wa masuala ya lishe. “Kuna mikoa inafanya vizuri mingine inasuasua, kuna halmashauri zinafanya vizuri lakini zingine zinasuasua,” alisema.

Hata hivyo, Jafo alisema hali ya usimamizi wa masuala ya lishe imeimarika tofauti na awali na kuwataka wakuu hao wa mikoa kuongeza mkazo.

Naye katibu mkuu wa ofisi hiyo Joseph Nyamhanga, alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao wa 2019/20 zimetengwa Sh50 bilioni kwa ajili ya lishe.



Chanzo: mwananchi.co.tz