Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar, Dodoma, Mwanza vinara wa mapato

919ea3ecd6fcdfb1ff8987c16bd2dc28 Dar, Dodoma, Mwanza vinara wa mapato

Fri, 22 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imewataka wakuu wa mikoa ambao halmashauri zao zimekusanya mapato chini ya asilimia 50 wafanye tathimini na kuweka mikakati ya kukusanya mapato zaidi katika vipindi vilivyosalia ili kufikia malengo ya mwisho wa mwaka.

Pia imewataka wakurugenzi wa halmashauri ambazo hazijafikia asilimia 50 ya makisio hasa walio chini ya asilimia 25 kwa kipindi cha nusu mwaka kwenye ukusanyaji ya mapato, kujitathimini kwa kina.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alitoa maagizo hayo jana jijini Dodoma wakati akitoa tarifa ya ukusanyaji mapato ya ndani ya halmashauri katika kipindi cha miezi sita (Julai-Desemba) mwaka jana.

Pia amezitaka halmashauri zisizotoa mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu ifikapo Jumatatu ijayo zipeleke barua ya maelezo ni kwa nini hazikufanya hivyo na ndani ya wiki mbili fedha hizo zitolewe.

"Mikoa ambayo halmashauri zake zimekusanya mapato chini ya asilimia 50 hazina budi kufanya tathmini na kuhakikisha zinaweka mikakati madhubuti ya kukusanya mapato katika vipindi vilivyosalia.”

"Wakurugenzi wa halmashauri ambazo hazijifikia asilimia 50 ya makisio kwa kipindi hiki cha nusu mwaka wanatakiwa kujitathmini na kuweka mikakati mizuri ya kufikia malengo mwisho wa mwaka hasa wasiofika asilimia 25," alisema.

Jafo alisema kwa mwaka wa fedha 2020/21 halmashauri zilipanga kukusanya Sh bilioni 814.96 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani na katika kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka jana zimekusanya jumla ya Sh bilioni 381.27 ambazo ni asilimia 47 ya makisio ya mwaka.

"Itakumbukwa kwamba bajeti ya makusanyo ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa iliongezeka kutoka Sh bilioni 765.483 mwaka wa fedha 2019/2020 hadi Sh bilioni 814.96 mwaka wa fedha 2020/2021," alisema Jafo.

Alisema uchambuzi wa taarifa za mapato ya vyanzo vya ndani vya halmashauri katika kipindi cha Julai - Desemba, mwaka jana umeonesha kuwapo kwa ongezeko la mapato yaliyokusanywa kwa kiasi cha Sh bilioni 24.5 sawa na asilimia saba ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2019.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Momba imeongeza jitihada katika ukusanyaji ikilinganishwa na kipindi kilichopita cha mwaka wa fedha 2019/20 ambacho ilikuwa ni halmashauri ya mwisho kwa asilimia ya makusanyo.

Jafo alisema katika kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka jana, halmashauri tatu zimekusanya kati ya asilimia 80 hadi asilimia 88 ambayo ni asilimia mbili ya halmashauri zote 185 na halmashauri 73 zimekusanya kati ya asilimia 50 hadi asilimia 79 ya makisio ya mwaka ambayo ni asilimia 39.

Aidha, alisema halmashauri 107 zimekusanya kati ya asilimia 20 hadi 49 ambayo ni asilimia 58 ya halmashauri zote na halmashauri mbili zimekusanya chini ya asilimia 20 ya makisio ya mwaka.

Waziri huyo alisema ufanisi wa halmashauri katika kukusanya mapato ya ndani kwa ujumla wake katika kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka jana, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 88 ya makisio yake ya mwaka na halmashauri za wilaya za Kishapu na Longido zimekuwa za mwisho kwa kukusanya chini ya asilimia 20 ya makisio yake ya mwaka.

Alisema pia katika kuzipima halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imekusanya mapato mengi zaidi kuliko halmashauri zote kwa kukusanya Sh bilioni 30.67 na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imekusanya mapato kidogo kuliko halmashauri zote kwa kukusanya Sh milioni 324.89.

Kuhusu hali ya ukusanyaji wa vyanzo vikuu vya mapato ya ndani, Jafo alisema hutambuliwa kutokana na asilimia ya uchangiaji wa kila chanzo katika jumla ya mapato yote ya ndani ya halmashauri.

Alisema kutokana na uchambuzi wa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani katika kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka jana, imebainika kuwa vyanzo vikuu vya mapato ya halmashauri ni ushuru wa huduma, ushuru wa mazao, ushuru wa leseni za biashara na mapato yatokanayo na uchangiaji wa huduma za afya.

Halmashauri 5 zilizoongoza kwa kigezo cha asilimia

Halmashauri tano zilizoongoza kwa kigezo cha asilimia ya mapato ya ndani yaliyokusanywa ni Masasi DC asilimia 88, Momba DC asilimia 81, Njombe DC asilimia 80, Hanang DC asilimia 75 na Nachingwea DC asilimia 73.

Halmashauri 5 zilizoongozwa kwa wingi wa mapato

Alizitaja halmashauri tano zilizoongoza kwa kigezo cha pato ghafi kuwa ni Ilala Sh bilioni 30.67 sawa na asilimia 51, Kinondoni Sh bilioni 21.83 sawa na asilimia 51, Dodoma Sh bilioni 18.53 sawa na asilimia 39, Temeke Sh bilioni 17.41 sawa na asilimia 52 na Arusha Sh bilioni 9.39 sawa na asilimia 43.

Halmshauri 5 za mwisho

kwa kigezo cha asilimia

Alizitaja halmashauri tano za mwisho kwa kigezo cha asilimia ya mapato ya ndani yaliyokusanywa ni Chamwino DC asilimia 23, Bariadi TC asilimia 23, Itilima DC asilimia 23, Longido asilimia 18 na Kishapu DC asilimia 16.

Halmashauri 5 za mwisho kwa wingi wa mapato

Halmashauri tano za mwisho kwa kigezo cha pato ghafi ni Siha DC Sh milioni 404 (asilimia 31), Longido DC Sh milioni 390 (asilimia18), Buhigwe Sh milioni 362 (asilimia 54), Kigoma Sh milioni 353 (asilimia 50) na Itilima Sh milioni 324 (asilimia 23).

Mikoa mitano iliyoongoza kwa kigezo cha asilimia

Waziri huyo aliitaja mikoa mitano iliyoongoza kwa kigezo cha asilimia ya mapato ya ndani yaliyokusanywa ni Katavi (asilimia 62), Manyara (asilimia 57), Songwe (asilimia 56), Geita (asilimia 55) na Njombe (asilimia 52).

Mikoa mitano iliyoongoza kwa wingi wa mapato

Mikoa mitano iliyoongoza kwa kigezo cha pato ghafi ni Dar es Salaam Sh bilioni 89.12 (asilimia 51), Dodoma Sh bilioni 24.44 (asilimia 40), Mwanza Sh bilioni 19.56 (asilimia 45), Mbeya Sh bilioni 19.43 (asilimia 48) na Pwani Sh bilioni 18.28 (asilimia 47).

Mikoa mitano ya mwisho

kwa kigezo cha asilimia

Aliitaja mikoa mitano ya mwisho kwa kigezo cha asilimia ya mapato ya ndani yaliyokusanywa kuwa ni Mara (asilimia 41), Tanga (asilimia 41), Dodoma (asilimia 40), Singida (asilimia 39) na Simiyu (asilimia 36).

Mikoa mitano ya mwisho

kwa wingi wa mapato

Mikoa mitano ya mwisho kwa kigezo cha pato ghafi (wingi wa mapato ya ndani yaliyokusanywa) ni Singida Sh bilioni 6 (asilimia 39), Kigoma Sh bilioni nne (asilimia 43), Katavi Sh bilioni tano (asilimia 62), Simiyu bilioni tano (asilimia 36) na Rukwa bilioni 4.07 (asilimia 43).

-----------------------------------------------------------------------------

Wizara yaagizwa kuwasiliana na Hazina deni la bil 22/- ANCHOR

Na Magnus Mahenge, Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iwasiliane na Wizara ya Fedha na Mipango ili taasisi za serikali zilipe Sh bilioni 22 wanazodaiwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL).

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Moshi Kakoso, deni hilo ni hadi Desemba mwaka jana na limetokana na huduma za simu na data.

Alisema hayo baada ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliyoundwa Desemba 5, mwaka jana kueleza muundo, mipango na majukumu ya wizara na taasisi zake.

"Taasisi za serikali zinazodaiwa na TTCL kiasi cha Sh bilioni 22 hadi Desemba, 2020 zilipe madeni yao kutokana na kutumia huduma walizopewa na TTCL za simu na data," alisema.

Kakoso alitaka pia wizara hiyo iwasiliane na Wizara ya Fedha na Mipango ili kuliondolea mzigo Shirika la Posta (TPC) la kulipa pensheni kwa wastaafu waliokuwa wfanyakazi wa Shirika la Posta na Simu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema shirika hilo tangu mwaka 2016 hadi sasa limeshalipa Sh bilioni 10 wastaafu hao.

Aidha, aliupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Mamlala ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuendelea kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi na kudhibiti matumizi ya huduma za mawasiliano na vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

Pia kamati hiyo ilimpongeza Waziri wa wizara hiyo, Dk Faustine Ndugulile kwa kuanza kuchukua hatua na kushughulikia changamoto na malalamiko ya wananchi wanaotumia vifurushi na bando za simu za mkononi zinazotolewa na kampuni za simu za mkononi.

Pia aliiitaka wizara hiyo kushughulikia mwingiliano wa mawasiliano kwenye maeneo ya mipakani ili wananchi waishio maeneo hayo waweze kupata huduma za mawasiliano bila kuingiliana na nchi jirani.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Zainab Chaula alisema wizara imekutana na kamati hiyo kwa mara ya kwanza na ipo tayari kushirikiana ili kuongeza msukumo wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba alisema wataendelea kujenga minara ili kufikisha huduma za mawasiliano kwenye maeneo ya mipakani, yenye milima na miinuko na watatumia teknolojia rahisi kuongeza wigo wa upatikanaji wa mawasiliano nchini.

Mjumbe wa kamati hiyo, Zuberi Kuchauka alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuunda wizara hiyo mpya kwa kuwa dunia imehamia kwenye mitandao, inajikita kwenye uchumi wa kidijitali na Tehama ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuchangia Pato la Taifa.

Kuchauka pia aliitaka wizara hiyo iwekeze kwenye tafiti za Tehama na kuwaendeleza wataalamu wake ili kutumia teknolojia kulinda usalama wa taifa kwenye mtandao.

----------------------------------------------------------------------

Gharama ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini kupunguzwa

Na Magnus Mahenge, Dodoma

WAZIRI wa Nishati, Dk Merdard Kalemani ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa wizara hiyo imeanza kuzifanyia kazi kanuni za ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini na kwenye miji midogo ili kupunguza gharama za ujenzi kutoka Sh milioni 500 wanazotozwa wawekezaji.

Alisema hayo wakati akitoa taarifa ya utendaji wa sekta ya nishati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma iliyokuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Seif khamis Gulamali.

Dk Kalemani alisema lengo la wizara hiyo ni kusambaza vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini na katika miji midogo lakini kanuni zimekuwa kikwazo.

"Katika kuhakikisha wizara inasambaza vituo vya mafuta vijijini na katika miji midogo, inazipitia kanuni ili kuzirekebisha na kupunguza gharama za uwekezaji wa ujenzi wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini na miji midogo kutoka Sh milioni 500 anazotakiwa kutoa mwekezaji," alisema.

Dk Kalemani alisema kanuni zikibadilishwa mpango wa wizara hiyo wa kuendelea kusambaza vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini na miji midogo kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa nishati ya mafuta na usalama kwa watumiaji wa maeneo tajwa yanayokabiliwa na upungufu wa mafuta utafanikiwa.

Alisema pia katika kufanikisha azma hiyo ya kusambaza vituo katika vijijini na miji midogo, wizara hiyo inafikiria kujenga vituo rahisi vya pampu moja katika maeneo hayo, ambavyo uwekezaji wake utakuwa nafuu.

Kuhusu mkakati wa wizara kusambaza umeme nchini, Dk Kalemani alisema wizara hiyo itahakikisha vijiji vyote 2,200 vilivyobakia ambavyo bado havijaunganishwa na umeme vinapatiwa huduma hiyo ndani ya miezi 18 kuanzia sasa.

Chanzo: habarileo.co.tz