Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daladala zinazoishia Kivukoni mwisho Oktoba 20

Kivukoni Daladala.png Daladala zinazoishia Kivukoni mwisho Oktoba 20

Mon, 9 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zaidi ya daladala 260 zilizokuwa zikifanya safari zake maeneo mbalimbali na kuishia kituo cha Kivukoni zimehamishwa na kupangia vituo vitatu sehemu tofauti jijini humo, utekelezaji utakaonza rasmi Oktoba 20.

Hatua hiyo imetangazwa leo Jumatatu Oktoba 9, 2023 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart), Willium Gatambi katika mkutano na waandishi wa habari.

Akizungumzia hilo Gatambi amesema daladala hizo zinahamishwa ili kupisha upanuzi wa kituo chao cha Kivukoni kwa ajili ya mapokezi ya mabasi yao yatakayoishia hapo kwenye ujenzi wa awamu ya tatu na ya nne utakaohusisha magari yatakayotoka Gongo la Mboto, Mbagala na Mwenge.

"Kuisha kwa ujenzi wa awamu hizi ni wazi kuwa kutakuwa na ongezeko la mabasi na hivyo kutulazimu kutanua zaidi kutuo chetu kuliko ilivyo sasa, ndio maana yanaanza maandalizi mapema,"amesema Gatambi.

Ametaja vituo ambavyo daladala hizo zitaishia kuwa ni pembezoni mwa ukuta wa Wizara ya Ardhi ikihusisha magari yanayotoka Kigogo Sokoni, Tabata Chang'ombe, Tabata Kinyerezi, Buyuni Sokoni na Machinga Complex.

Kituo kingine Gatambi amesema ni NBC maarufu Posta ya Zamani. Hiki kitahusisha daladala zinazotoka Kisemvule, Kivule Sokoni na Mbande Kisewe.

Wakati kituo cha tatu kitakuwa ni Mtaa wa Ohio kikihusisha daladala zinazotoka Gongo la Mboto na Tegeta Nyuki.

"Hata hivyo mabadiliko hayo hayatazigusa bajaji kwani zenyewe zitakuwa zikiegesha pembezoni mwa uzio utakaowekwa wakati ujenzi ukiendelea," amesema Gatambi.

Kaimu Meneja wa mipango ya Usafirishaji wa Dart, Mhandisi Mohammed Kuganda amesema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya barabara za mabasi yaendayo haraka awamu ya tatu na ya nne ikihusisha barabara ya Bibi Titi, Ali Hassan Mwinyi na Sam Nujoma ambapo kila barabara itakuwa na mkandarasi wake.

"Kukamilika kwa awamu hizi za ujenzi wa barabara pamoja na awamu ya tano na ya sita utakifanya kituo cha Kivukoni kuhudumia zaidi ya mabasi yetu 3,200, hivyo utaona namna gani kunahitajika eneo kubwa na la kutosha kuingia mabasi hayo," amesema Kuganda.

Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam Darcoboa), Shifwaya Lema amesema wanashukuru wameshirikishwa katika mchakato mzima wa kuhamishwa eneo hilo na kuwaomba radhi abiria kwa usumbufu watakaoupata kwa kuwa ni moja ya mikakati ya Serikali katika kurahisisha hali ya usafiri nchini.

Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhinini (Latra) Mkoa wa Dar es Salaam, Rahim Kondo amewataka madereva wa daladala za njia zilizotajwa kuheshimu maelekezo na kueleza kuwa hatarajii kuona zikikatisha safari na kuleta usumbufu kwa abiria.

Mtendaji Kata ya Kivukoni, Aristides Balile ameomba watumiaji wa vituo vilivyopaangwa kuhakikisha wanaheshimu maeneo hayo kwa kuwa ni maeneo maalumu (smart area), ikiwemo kuepuka kuchafua mazingira kwa kuwa kutakuwepo na vifaa vya kutosha vya kuhifadhia taka.

Baadhi ya abiria wakizungumzia mabadiliko hayo, akiwemo Razia Amri, amesema anaona inavyoenda kumuongezea gharama za usafiri kwa kuwa awali alizoea kupanda gari moja kutoka Gongo la Mboto, sasa atalazimika kuchukua na bajaji kifika huko ambazo gharama yake ni kati ya Sh500 hadi Sh1000.

"Sisi tunaoenda kuchukua samaki kurudi kwa daladala Kivukoni kulitusaidia sana, sasa ni wazi tunaenda kubeba mizigo hii kichwani kwani itakuwa haitulipi," amesema Diana Ambrose mfanyabiashara wa samaki na mkazi wa Tabata Chang'ombe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live