Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daladala zagoma saa nane kushikiza bajaji ziondolewe

22415 Pic+daladala TanzaniaWeb

Tue, 16 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Wananchi wengi wa Manispaa ya Morogoro wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari jana walilazimika kutembea kwa miguu na wengine kupanda na vyombo vingine vya usafiri visivyoruhusiwa kisheria kupakia abiria yakiwamo malori baada ya daladala kugoma kutoa huduma kushinikiza kuondolewa kwa bajaji.

Mgomo huo ulioanza mapema alfajiri, ulilenga kuishinikiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kuondoa usafiri wa bajaji kwenye barabara zinazotumiwa na daladala na pia kupandisha nauli kutoka Sh400 hadi 500.

Mwenyekiti wa umoja wa madereva wa daladala katika Manispaa ya Morogoro, Joseph Mazuma alitaja sababu nyingine za kufanya mgomo huo kuwa ni kupinga unyanyasaji wanaofanyiwa na baadhi ya askari wa usalama barabarani wa kutozwa faini zaidi ya mara mbili kwa kosa moja.

Mazuma alisema bajaji zinasafirisha abiria hata kwenye barabara zenye daladala za kutosha, jambo ambalo linawafanya madereva wa mabasi hayo kushindwa kupakia abiria na kukamilisha hesabu ya mmiliki kwa siku.

Alisema zipo baadhi ya barabara ikiwamo ya Kilakala, madereva wa bajaji wamezivamia na kufanya shughuli ya kusafirisha abiria hali inayosababisha wenye daladala kuacha kwenda ruti hiyo.

Alisema zipo pia oparesheni zinazofanywa na Sumatra kwa kushirikina na polisi alizodai kuwa zina lengo la kudhoofisha usafiri wa daladala na tayari suala hilo lilishajadiliwa na uongozi wa umoja wa madereva na viongozi wa Sumatra na Serikali kulizungumzia, lakini bado zinaendelea.

Alisema Sumatra na polisi wamekuwa wakiwaandama madereva wa daladala na kuwaacha wa bajaji wakivunja sheria nyingi za usalama barabarani bila ya kuwachukulia hatua.

Msimamo wa madereva wa daladala umeonekana kuwa na baraka za wamiliki ambao wameiomba Serikali kuweka utaratibu mzuri wa usafirishaji abiria kwa vyombo vilivyoruhusiwa kisheria ili kuepuka mgongano wa kimasilahi ambao unawaathiri wananchi na uchumi kwa ujumla.

Mmoja wa wamiliki hao, Amari Juma alisema kiwango cha nauli ya daladala kilichopo sasa hakiendani na hali halisi ya uendeshaji wa biashara ya usafirishaji hasa ikizingatiwa kuwa bei ya petroli imepanda hadi kufikia Sh2393 kwa lita moja.

Juma alisema licha ya kuibuka kwa kasi kwa usafiri wa bajaji, lakini usafiri wa daladala bado una nafasi kubwa na una umuhimu katika sekta ya usafirishaji hivyo lazima Serikali iweke mipango na utaratibu mzuri utakaokuwa na masilahi kwa madereva na wamiliki wa daladala.

Akizungumzia madai ya madereva hao, Kaimu Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Morogoro, Maria Chacha alisema kitendo cha madereva wa bajaji kufanya shughuli za usafirishaji abiria kama daladala ni kinyume cha sheria na hatua za kisheria zitachukuliwa kuanzia sasa.

Hata hivyo, aliwataka madereva wa daladala kujitathmini na kujiuza kwa nini abiria wanakimbilia bajaji ambazo zinatoza nauli kubwa badala ya daladala.

Alisema daladala nyingi zimekuwa zikichelewa kwenye vituo, hivyo abiria wanashindwa kuvumilia na kuamua kupanda bajaji na nyingine zinajaza abiria kupita kiasi huku madereva na makondakta wakiwatolea abiria lugha chafu.

Kupanda kwa nauli

Kuhusu kupandisha nauli, Maria aliwataka wamiliki wa daladala kupitia umoja wao, kuandika barua ya kuomba kupandisha nauli ili taratibu zifuatwe akisisitiza kuwa uamuzi wa kupandisha nauli si wa siku moja na hautolewi na mtu mmoja.

Mei 9, mwaka juzi, madereva na wamiliki wa daladala walifanya mgomo kama wa jana wakishinikiza kuondolewa kwa Ofisa wa Sumatra Mkoa wa Morogoro, Rahim Kondo kwa kile walichodai kuwa amekuwa akiwanyanyasa madereva kwa kuwatoza faini kinyume cha sheria.

Mgomo huo wa siku mbili ulimfanya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk Stephen Kebwe kumsimamisha afisa huyo ambaye baadaye alihamishiwa makao makuu ya Sumatra.

Chanzo: mwananchi.co.tz