WATU watano wamekufa na wengine 10 wamejeruhiwa katika ajali ya magari iliyotokea kwenye makutano ya barabara za Chang’ombe na Mandela, Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam alfajiri jana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Amon Kikwale, alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea saa 9:45 usiku wa kuamkia jana ikihusisha magari matatu likiwemo daladala linalofanya safari kati ya Temeke-Muhimbili na malori mawili.
Alisema, gari lenye namba za usajili T 700 DKY Nissan Civilian (daladala) lililokuwa linakwenda Muhimbili liligongana na lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 920 CQP na tela lenye namba T 460 CEX ambalo nalo liligongwa na lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 536 CFC.
Kamanda Kikwale aliwataja majeruhi kwenye ajali hiyo kuwa ni Zuhura Rajabu (50) mkazi wa Tandika, Rukia Chande (32) mkazi wa Yombo Makaburini, Martias Msapa (21) mkazi wa Buza na Halis Msafiri (25) mkazi Yombo.
Wengine ni Richard Oswad (22) mkazi wa Buza, Hamad Kanda (28) mkazi wa Tandika, Emmanuel Brown (26) mkazi wa Buza na Shida Salum (24) mkazi wa Temeke.
Kamanda Kikwale alisema, miili ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke, na pia majeruhi wote walikimbizwa hospitalini hapo.
Alisema baada ya ajali hiyo madereva wawili walikimbia isipokuwa dereva wa lori namba T 536 CFC Scania lililokuwa likitoka Sokota kwenda Uhasibu, Alphonce Raphael.
“Nawaomba madereva watambue kuwa wamebeba roho za watu, hii ni ajali mbaya kuwahi kutokea hapa Temeke tena imetokea kwenye mataa ni ishara kuwa taa hizi hazikuzingatiwa,” alisema Kamanda Kikwale.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke Meshack Shimwela, alisema hospitali ilipokea majeruhi na maiti waliotokana na ajali hiyo.
“Tulipokea majeruhi wengi na watu watano walikuwa wameshafariki. Majeruhi tuliopokea walikuwa na hali mbaya na kazi kubwa tuliyofanya ni kuwa stabilize ambapo wanne tumewapeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa tiba zaidi,” alisema Dk Shimwela.
Awali, akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema uchunguzi wa awali, umeonesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa daladala ambaye alipita kwenye taa bila kuzingatia usalama.
Alisema walimhoji mmoja wa majeruhi ambaye ni Oswadi aliyebainisha kuwa abiria walijaribu kumuonya dereva lakini aliwaeleza wasiingilie kazi yake.