Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DPP apewa siku 3 kuwajibu wafugaji

Mifugo DPP DPP apewa siku 3 kuwajibu wafugaji

Wed, 20 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) amepewa siku tatu kuwasilisha majibu kinzani ya kiapo cha wafugaji wawili ambao wameweka zuio la kuuzwa kwa mnada kwa mifugo yao 1,448 iliyokamatwa wilayani Siha wiki mbili zilizopita.

Wakati Jaji Safina Semfukwe wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi akitoa amri hiyo jana, wafugaji hao, wameeleza katika hati ya kiapo kuwa mifugo yao hiyo ilivunja boma walikokuwa wamehifadhiwa Julai 2, 2022 na kuelekea kusikojulikana.

Ng’ombe hao 485 na jumla ya kondoo na Mbuzi 963, walikuwa wauzwe kwa mnada jana kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Siha, iliyotolewa Julai 12, 2022 kabla ya kuzuiwa na Mahakama Kuu kutokana na maombi ya wafugaji hao.

Juzi maombi ya wafugaji hao wanaotetewa na wakili Elia Kiwia, yalitajwa mbele ya Jaji Simfukwe ambaye alimtaka DPP na mjibu maombi wa pili, Newton Makwale kuwasilisha kiapo kinzani ndani ya siku tatu na kesi itatajwa Julai 21.

Hata hivyo, idadi ya mifugo inayoonekana kwenye hukumu ya Hakimu Mkazi Siha, Jasmin Abdul ya 1,448 kwa maana ya ng’ombe 485 na mbuzi na kondoo 963, inatofautiana na iliyopo kwenye hati ya kiapo ya mbuzi 1,300 na ng’ombe 485.

Related Mahakama yazuia uuzwaji mifugoAdvertisement Walichoeleza wafugaji

Katika hati ya kiapo chao, wafugaji hao, Sinjore Laizer na Isaya Mollel wameieleza mahakama kuwa wao ndio wamiliki wa mbuzi 1,300 na ng’ombe 485 ambao maombi ya kuwataifisha yaliwasilishwa mahakama ya Siha na kutolewa uamuzi.

Wanaeleza kuwa Julai 2, 2022, huko nyumbani kwao Lerai wilaya ya Longido, mifugo iliyotajwa ilivunja uzio wa eneo walimokuwa wanatunzwa na kwenda kusikojulikana na jitihada za wanakijiji kuwatafuta hazikuzaa matunda.

Kupitia kwa wakili Kiwia, wanadai baada ya siku mbili tangu kutoweka kwa mifugo yao, walikwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi cha Olmolog lakini wakawaambia wanaweza kuwa wamechanganyika na makundi mengine ya mifugo.

Wafugaji hao wanaeleza polisi hao waliwataka waendelee kutafuta mifugo yao na Julai 13, 2022 walikwenda kituo cha Polisi Sanyajuu kuulizia kama wameiona mifugo hiyo na waliwaambia ilipatikana na inahifadhiwa shamba la Narco Siha.

Wanaeleza katika kiapo hicho kuwa, polisi hapo waliwaeleza kuwa baada ya mifugo hiyo kukutwa ikirandaranda katika mashamba ya milimani huko West Kilimanjaro, walimjulisha mjibu maombi wa kwanza (DPP) kwa hatua zaidi.

Kulingana na kiapo hicho, wafugaji hao wanasema polisi hao walienda mbali na kuwajulisha kuwa suala hilo lilishafunguliwa shauri mahakama ya Hakimu Mkazi Siha na kutolewa uamuzi kuwa mifugo hiyo iuzwe kwa mnada wa hadhara.

Wafugaji hao wanadai kulikuwapo na ukiukwaji wa taratibu za kisheria, hivyo Mahakama Kuu ilipaswa kuingilia kati na kwamba hawakupewa haki ya asili ya kusikilizwa na hivyo ili kutenda haki, ni vyema na wao wakasikilizwa.

“Tuko tayari kuweka dhamana au wadhamini kwa masharti yatakayowekwa na mamlaka yoyote ili mifugo iachiwe na kuwa chini ya uangalizi wetu katika kipindi chote cha uchunguzi wa suala hilo,”walisema.

Maombi ya DPP yalivyokuwa

Mara baada ya kukamatwa kwa ng’ombe hao, DPP akiwakilishwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Kassim Nassir akisaidiwa na mwendesha mashitaka, David Chishimba walifungua maombi ya jinai namba 17 ya mwaka 2022.

Katika maombi hayo yaliyosikilizwa na Hakimu Mkazi Siha, Jasmin Abdul, waliomba mambo mawili, moja ni mahakama itoe amri ya kukamatwa, kuzuiwa na kutaifishwa kwa ng’ombe 485 na mbuzi na kondoo wapatao 963.

Pia wakaiomba mahakama iteue dalali wa kuuza kwa mnada wa dharura mifugo hiyo na kwamba fedha zitakazotokana na mauzo hayo ziingizwe katika akaunti yenye jina la DPP iliyopo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Akiwasilisha hoja za maombi hayo, wakili Nassir alisema mifugo hiyo iliingizwa kwa jinai katika mashamba ya wakulima katika kijiji cha Olmolog na kwamba mbali na kuingizwa kwa jinai, ilikiuka sheria udhibiti magonjwa ya wanyama.

Wakili Nassir alisema mifugo hiyo inatoka nje ya wilaya ya Siha na mkoa wa Kilimanjaro na iliingizwa katika mkoa huo bila vibali vya maofisa mifugo kwa mujibu wa sheria ya magonjwa ya mifugo ya mwaka 2003.

Mbali na hoja hiyo, lakini alisema mifugo ililishwa katika mashamba ya wakulima yenye mazao aina ya njegere, ngano, mbaazi na mazao mengine na kwamba hadi anawasilisha maombi hayo, hakuna aliyejitokeza na kudai kuwa ilikuwa ni mifugo yake.

Wakili Nassir aliieleza mahakama kuwa mifugo hiyo ilikuwa inahifadhiwa katika shamba la Ranchi ya Taifa (Narco) wilayani Siha ambalo halina miundombinu ya kutosha na wafanyakazi na inaweza ikafa kwa kukosa huduma endelevu.

“Waathirika (wakulima) ambao mazao yao yaliharibiwa wanategemea kuuzwa kwa mifugo hiyo ili waweze kufidia hasara waliyoipata,”alieleza wakili huyo.

Akitoa uamuzi wake, Hakimu Jasmin alisema alifika eneo inapotunzwa mifugo hiyo na kushuhudia yale aliyoyasema wakili Nassir na kuongeza kuwa ameshuhudia eneo hilo linakabiliwa na ukame.

Hakimu huyo alisema ukame huo unaweza kusababisha ng’ombe kufa kama hatua za haraka hazitachukuliwa.

Kwa mujibu wa hakimu huyo, hadi anapoandika uamuzi huo Julai 12, hakuna mtu aliyekuwa amejitokeza kudai kuwa ni mmiliki halali.

Hakimu Jasmin alitoa amri ya kutaifishwa mifugo hiyo na akamteua Newton Makwale kuwa dalali wa kuiuza kwa dharura na fedha zitakazopatikana ziingizwe kwenye akaunti ya DPP iliyopo BoT.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live