Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DED, ofisa usalama wa wilaya wadaiwa kuchapana makonde

37239 Pic+ded DED, ofisa usalama wa wilaya wadaiwa kuchapana makonde

Fri, 18 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanga. Mgogoro wa kiuongozi, umeendelea kuitesa Wilaya ya Mwanga, baada ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Zefrin Lubuva kudaiwa kupigana na ofisa usalama wa wilaya, Abdi Mussa katika ofisi ya mkurugenzi huyo.

Tukio hilo linalodaiwa kutokea jana mchana limeibuka siku chache baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Aaron Mbogho kumuweka ndani Lubuva kwa madai ya kushindwa kutekeleza maagizo yake.

Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo, ambao hawakutaka kutajwa gazetini walisema kwamba awali, asubuhi kulikuwa na kikao katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, ambacho kilihitaji uwepo wa mkurugenzi huyo, lakini hakuhudhuria na badala yake alimtuma mwakilishi wake, jambo ambalo linadaiwa kuwa halikumfurahisha ofisa usalama huyo ambaye baadaye aliamua kumfuata ofisini kuhoji kwa nini hakuhudhuria kikao.

“Katika kikao hicho, ofisa usalama alimtaka mkurugenzi mwenyewe ashiriki na alipotuma mwakilishi, ndipo shida ilipoanzia, maana alitoka na kumfuata ofisini, na katika majibizano ya maneno, pakatokea kutokuelewana na kuanza kurushiana ngumi” alidai mmoja wa watumishi hao. Alipoulizwa kuhusu tukio hilo Lubuva hakutaka kulizungumzia kwa undani, badala yake alisema anaziachia mamlaka husika zifanye kazi yake.

Hata hivyo, Mussa alikana madai hayo akisema kwa kifupi, “Si za kweli.”

Alipoulizwa, Mbogho, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya alisema, “Mimi mwenyewe nimelisikia kama wewe ulivyolisikia. Nimeambiwa DED yuko polisi sijui nini kimetokea. Nipe muda nifuatilie nikipata taarifa kamili nitawajulisha,” alisema Mbogho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alipoulizwa kwa simu kuhusu taarifa hizo alisema, “Hii taarifa ni ya wilayani hivyo siijui na wala haijanifikia ofisini kwangu.”



Chanzo: mwananchi.co.tz