Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DED awakumbusha wahakiki kaya maskini

65e919d3c78711843791eed367059d2a DED awakumbusha wahakiki kaya maskini

Thu, 10 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa katika mkoani Dodoma, Dk Omary Mkulo amewataka wasimamizi wa kuhakiki mradi wa Kunusuru Kaya Maskini Nchini (Tasaf) Awamu ya III kufanya kazi kwa umakini na uaminifu ili fedha hizo ziwafikie walengwa wenye sifa.

Dk Mkulo alitoa kauli hiyo kwenye mafunzo ya siku moja kwa wasimamizi wa kuhakiki kaya maskini kwa awamu ya pili kwenye halmashauri hiyo.

Aliwataka wasimamizi hao kutenda haki na kuzibaini kaya hizo zitakazostahili kuingia kwenye mpango huo wa serikali wenye nia ya kuzikomboa kiuchumi.

"Ndugu zangu uhakiki huu ni muhimu kwa sababu tukienda kinyume tunaweza kuingiza watu wasio na sifa, na wakiingia watu ambao hawana sifa tafsiri yake ni kwamba wataendelea kupokea fedha za serikali ambayo ingewasidia watu masikini," alisema.

Aliongeza kuwa, “Ukiiacha kaya maskini halafu ukaingiza kaya yenye uwezo, yaani hata kwa Mungu utakuwa hujatenda haki kwa sababu tutakuwa tumwemwacha yule ambaye anastahili kuwepo kwenye mpango huo."

Aidha, aliwataka kusimamia uhakiki huo kwa makini na kuziondoa kaya ambazo zimekosa sifa ya kuendelea kupokea ruzuku hiyo

Ofisa Ufuatiliaji na Ushauri Mradi wa Tasaf Wilaya ya Kongwa, Sopi Samwel alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watoa huduma kabla ya kuanza uhakiki awamu ya pili kuanzia Desemba 8 hadi 11 mwaka huu.

Samwel alisema uhakiki huo unaendeshwa nchi nzima kwa mikoa iliyobaki ya Tanzania Bara na Visiwani. Tayari mikoa 12 ya Tanzania Bara imekamilisha uhakiki awamu ya pili. Mikoa hiyo hiyo ni Mwanza, Kagera, Rukwa, Katavi, Simiyu, Shinyanga, Songwe, Mbeya, Mara, Kigoma, Tabora na Geita.

Alibanisha kuwa awamu ya kwanza ya uhakiki, ilifanyika kuanzia Julai mpaka Septemba mwaka huu. Alitaja lengo la serikali kufanya awamu ya pili ya uhakiki ni kutoa fursa kwa kaya zilizoachwa, kutokana na kutokuwepo wakati wa uhakiki awamu ya kwanza.

Alisema wasimamizi 20 waliopata mafunzo hayo, watashiriki kwenye kurudia uhakiki walengwa wa mpango wa Tasaf Awamu ya Pili kwa vijiji 43 vya wilaya ya hizo.

Mratibu wa Tasaf Wilaya ya Kongwa, Unambwe Erasto alisema katika uhakiki wa awamu ya kwanza kaya maskini 6,905 zilihakikiwa, lakini 6,656 ndizo zilikuwa na sifa ya kuendelea kupata ruzuku hiyo.

Erasto alisema baada ya kuhakiki, uhawilishaji wa fedha ulifanyika na kaya hizo zimepokea Sh milioni 466.3 kuanzia Septemba hadi Desemba mwaka huu.

Chanzo: habarileo.co.tz