Serengeti. Waswahili wanasema weka akiba ya maneno kwa sababu unayemtuhumu huwezi kujua ukaribu au cheo atakachokuwa nacho maishani.
Ukweli wa msemo huo unaonekana sasa baada ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Juma Hamsini kukumbushia tuhuma alizotupiwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Marwa Chacha alizotoa mbele ya Rais John Magufuli akidai ni mwizi.
Septemba 6, Rais Magufuli akiwa ziarani wilayani hapa, Chacha aliyekuwa mbunge Jimbo la Serengeti kupitia Chadema alidai Hamsini ni mwizi na kama hataondolewa maendeleo hayawezi kusonga.
Kauli hiyo ilijibiwa na Hamsini baada ya kupewa nafasi na Rais Magufuli na kudai taarifa hizo ni uongo kwani ‘mikono’ yake ni misafi, huku akidai amepata ugonjwa wa moyo wilayani hapo kutokana na majungu na vurugu hasa za kisiasa.
Kutokana na majibu hayo, Rais Magufuli huku akishangiliwa alimsafisha na kumshambulia Marwa kuwa hata hajachangia miradi na kumuomba mkurugenzi huyo kuchapa kazi na hatamtoa huku akitoa utani kuwa dawa yake ni kuoa dada zake ili amheshimu.
Akitoa shukrani baada ya kuzinduliwa mradi wa ushirikishwaji fedha, kuboresha usafi wa mazingira na afya Tanzania (Finish Fort) unaotekelezwa na Amref Health Africa, Aqua for All na kampuni ya Waste kwa ajili ya uchimbaji vyoo kaya 7,000 kwenye kata 11, Hamsini alisema wilaya hiyo hawana fadhila.
“Hata miradi inayoletwa na wafadhili viongozi wanakuwa wa kwanza kutoa taarifa zisizo sahihi,” alisema Hamsini.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa vitongoji kutoka Chadema waliohudhuria uzinduzi huo hawakusita walisikika wakisema: “Hata hivyo, kazi ulishamaliza akahamia CCM.”
Hamsini alisema: “Nilikuwa likizo sasa shemeji yenu nimerudi, nina mambo mengi ikiwamo uchaguzi, jamani uchaguzi upo na mimi ndiye msimamizi mkuu na utafanyika Desemba 2.” Hata hivyo, baadhi ya viongozi walionekana kukerwa na kauli yake kuhusu Marwa kwa kuwa suala lilimalizwa na Rais na hapakuwa na sababu kuliweka kwenye kadamnasi ilhali ndiye mgombea pekee wa ubunge kupitia CCM.
“Hivi huyu kama ana hasira hivi watafanyaje kazi na Ryoba akishinda ubunge ili walete maendeleo waliyokuwa wanadai yanakwamishwa na siasa za Chadema, lazima apime nini cha kusema kwa watu,” alisema mmoja wa watendaji kata ambaye hakutaka kutajwa jina.
Hata hivyo, mkuu wa wilaya hiyo, Nurdin Babu hakutaka kuzungumzia kauli hiyo licha ya kuwa mgeni rasmi.