Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC wa Mwanga amtupa mahabasu DED saa 24

35319 Pic+ded DC wa Mwanga amtupa mahabasu DED saa 24

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aron Mbogho ameamuru kuwekwa mahabusu kwa saa 24, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo (DED), Zefrin Lubuva akimtuhumu kufanya makosa mbalimbali.

Mbali na Lubuva, adhabu hiyo imemkumba pia kaimu mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mwanga, Justine Valentino.

“Ni kweli huyo mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga na kaimu mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mwanga wako mahabusu hivi tunavyoongea,” alisema Mbogho.

Alipoulizwa sababu za kuchukua uamuzi huo dhidi ya mkurugenzi huyo, Mbogho alisema “Wewe elewa tu kuwa yuko ndani mahabusu ya Kituo cha Polisi Mwanga.”

Baadaye alituma taarifa akisema ameshawakabidhi kwa Takukuru viongozi hao kwa hatua zaidi.

Wakati Mbogho akigoma kutaja sababu hizo, taarifa zinadai miongoni mwazo ni uamuzi wa mkurugenzi huyo kugoma kutekeleza maagizo ya mkuu huyo wa wilaya. “Huyo mkurugenzi alim-demote (kumshusha cheo) mweka hazina wa halmashauri, DC (mkuu wa wilaya) akaingilia kati kwa vile mkurugenzi hana mamlaka ya kufanya hivyo,” kilidokezwa chanzo cha habari hii.

Chanzo hicho kilidai kuwa baada mkurugenzi kumshusha cheo mweka hazinahuyo, alimpangia kwenda kuwa mhasibu katika mojawapo ya vijiji vya wilaya hiyo, jambo lililopingwa na Mbogho.

“Mkuu wa wilaya akamwagiza mkurugenzi kwanza atengue uamuzi wake kwa vile hana mamlaka hayo, lakini pia amrudishe kwenye wadhifa wake, lakini akawa hataki kufanya hivyo,” imeelezwa.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, mkuu wa wilaya alikasirika kupuuzwa kwa maagizo yake ndipo jana alipoamuru mkurugenzi huyo awekwe mahabusu kwa saa 24.

Hata hivyo, bado haijafahamika mara moja kwa nini mkurugenzi huyo amewekwa mahabusu pamoja na mtendaji wa mamlaka ya mji Mdogo wa Mwanga.

Mkuu huyo wa wilaya ameshawaweka mahabusu zaidi ya viongozi akiwamo Katibu Tawala wa Wilaya ya Mwanga (Das), Yusuph Kasuka Agosti jana.

Mwingine ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga, Jaffary Kandege ambaye alimwekwa mahabusu Mei, mwaka jana.

Mbogho alimtuhumu Kandege kufanya uchochezi na kusababisha maofisa wa Serikali waliokuwa wakipambana na uvuvi haramu kushambuliwa na wananchi.

Mwenyekiti huyo alikanusha tuhuma hizo na kudai mgogoro wao ulitokana na DC kukataa kutoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM (2015-2020) kwa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Mwanga.

Alipoulizwa jana jioni kuzungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Josephat Kandege alisema bado anafuatilia na kuahidi kutoa taarifa mara ya kupata maelezo ya kutosha.



Chanzo: mwananchi.co.tz