Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Sakina Mohamed amekemea biashara ya madereva malori kuuza mafuta barabarani kwa magendo maarufu kama ‘Kupiga nyoka’ wilayani humo huku akitaja kitendo hicho ni uhujumu uchumi.
Mkuu huyo wa Wilaya ameyasema hayo leo Alhamisi Oktoba 19, 2023 wakati wa muendelezo wa ziara zake ya kuwatembelea wachimbaji wa madini kwenye migodi iliyoko ndani ya wilaya hiyo pamoja na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Mbogwe.
"Biashara hii ni haramu, mafuta hayo yanapelekwa maeneo ya migodi kinyume na taratibu na kupelekea serikali kukosa mapato ambayo yangepatikana kama mafuta hayo yangepatikana kwenye vituo rasmi,”amekemea DC Sakina.
DC Sakina ameongeza kuwa biashara hiyo pia ina madhara kiafya kwakuwa watoto na wananchi kwa ujumla wanayanyonya mafuta hayo kwa mdomo na kujaza kwenye madumu.
Mbali na hilo, DC Sakina, amewataka wamiliki wa migodi hiyo kutoruhusu watoto walio chini ya miaka 18 kufanya kazi eneo hilo kwani ni kinyume na sheria ya watoto na inasababisha wengi wao kuacha shule.
"Waacheni watoto waende shule, kama mnataka pambaneni na watu wazima wenzenu mchukue majukumu badala ya kuwadanganya watoto na kuwaachisha shule,"amesema.
DC Sakina pamoja na Kamati ya Usalama Mbogwe wanaendelea na ziara katika Wilaya hiyo yenye malengo ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.