Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC awatuliza Ubungo bomoabomoa

F9035ee3dd5dad6ce9be1e8d05e59d60.jpeg DC awatuliza Ubungo bomoabomoa

Tue, 20 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WANANCHI wa Kimara mkoani Dar es Salaam ambao nyumba zao zipo katika mpango wa kuvunjwa kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro, wametakiwa kuwa watulivu wakati suala la ubomoaji wa nyumba hizo likishughulikiwa.

Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja kilichowakutanisha wananchi hao na Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Herry James alisema kilio cha wananchi hao kipo chini ya ofisi yake.

Awali Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam ulitoa siku 30 kwa wananchi hao kuondoka maeneo yao ili nyumba zivunjwe kupisha upanuzi wa barabara hiyo, suala ambalo wananchi hao wamelipinga.

Kwa mujibu wa wananchi hao, mbali ya siku zilizotolewa kuwa chache, pia baadhi yao wamedai kuwa mita 90 ambazo Tanroads imewataka kuzipisha ni nyingi tofauti na mita 60 ambazo wengi wanadai kuwa ndiyo zipo katika utaratibu.

Akizungumzia kuhusu suala hilo, James alisema tayari ofisi yake imelichukua suala hilo na kulifikisha katika Ofisi ya Tanroads ya Mkoa ambao kwa nafasi yao pia wamelipeleka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ili lipatiwe ufumbuzi hususani kuhusu kuongezwa muda wa wakazi hao kuhama tofauti zile siku 30.

“Baada ya kupokea malalamiko haya niliwasiliana na Tanroads ili kuongeza muda wa kuendelea kuwepo maeneo yenu ili kupata muda zaidi wa kujipanga,” alisema James.

Aidha, alisema baada ya kulishughulikia suala hilo kwa upande wa muda wa wananchi hao kuendelea kuwa maeneo hayo, muda wowote kuanzia sasa atakutana na wawakilishi wa wananchi hao ili kuzungumzia changamoto zingine zinazowakabili wananchi hao.

Mbunge wa Ubungo ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila alimshukuru mkuu wa wilaya hiyo kwa kulisimamia suala hilo huku akiahidi kukutana na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho ili kupata ufunguzi zaidi kuhusu suala hilo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz