Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC awataka wasafirishaji kuacha kutumia njia za panya

Njia Pic Data DC awataka wasafirishaji kuacha kutumia njia za panya

Wed, 31 Aug 2022 Chanzo: Mwananchi

Wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa majini watakaotumia bandari ya Karema wilayani Tanganyika pindi itakapoanza kazi wametakiwa kulipa ushuru na kodi ili iweze kujiendesha.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Agosti 31, 2022 na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu katika kikao cha wadau wa bandari kuhusu kuweka mikakati ya kuanza kufanya kazi.

Buswelu amesema wafanyabiashara wenyewe waliomba ijengewa bandari na ahadi hiyo serikali imetekeleza, hivyo wasipitishe boti kwenye bandari bubu kukwepa kodi.

Amesema bandari hiyo imetengenezwa kwa usanifu mkubwa ili kuinua uchumi wa Mkoa na Watanzania kwa ujumla iliyogharimu Sh47.9 bilioni ikitarajiwa kuanza kazi Septemba Mosi 2022.

 “Rai yangu kwa wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo waanze kuleta leo kwa maandalizi ya kusafirisha na inayoletwa ishushiwe hapa tumekubaliana na wadau,” amesema Buswelu.

Advertisement “Kamati za usalama wilaya na mkoa zimejipanga kuhakikisha shughuli zote zinazofanyika katika mazingira salama na taasisi zinazohusika zipo tayari,”amefafanua Buswelu.

Meneja wa Mamlaka ya Bandari Ukanda wa Ziwa Tanganyika, Edward Mabula amesema Bandari  ya Karema ina ukubwa wa mita 150 na kina cha mita 6.5 ambapo ina uwezo wa kupaki meli mbili kubwa.

“Ukubwa wa eneo ni hekta 66, zilizojengwa miundombinu ni ekari 15 pekee. Mamlaka ya bandari tupo tayari tumeleta vifaa vya kutosha tunaomba ushirikiano kwa wadau,”amesema Mabula.

Diwani wa Kata ya Karema kwa niaba ya wananchi Maico Kapata amesema wanatoa shukrani na upendo wa dhati kwa Rais (Samia Suluhu Hassan) kuwaletea mradi huo utabadilisha maisha yao.

“Watu walikuwa wanapanda boti zinazama, kwa sasa watafanya vizuri, maeneo yanayotaka kuthaminiwa wagawiwe wafanyabiashara wajenge maduka, halmashauri itenge eneo la biashara,” amesema Kapata.

Baadhi ya wafanyabiashara Joseph Lugeze na Mohamed Amur wamesema uwepo wa bandari hiyo utapunguza gharama za usafirishaji mizigo.

“Tumeambiwa  bandarini gharama ya kupakia mzigo ni Sh6,900 awali tulitumia Sh10,000 hadi Sh12,000, wakati wa kupakia au kushusha kwenye mitumbwi midogo  inazama tunapata hasara,”amesema Lugeze.

Ikumbukwe kuwa Bandari ya Karema imeanza kujengwa mwaka 2019 na itaanza kutumika Septemba 1, 2022 huku ikisubiriwa kuzinduliwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan mwezi ujao.

Chanzo: Mwananchi