Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC awasweka mahabusu mafundi, viongozi wa vijiji

Mbaroniiiiiiiii DC awasweka mahabusu mafundi, viongozi wa vijiji

Sun, 7 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo ameamuru mafundi na wasimamizi, wakiwemo viongozi wa Serikali za mitaa wanaosimamia utekelezaji wa miradi ya ujenzi ya miundombinu ya elimu katika vijiji vya Lwenga na Nyamikoma waswekwe mahabusu.

Shimo amefikia hatua hiyo kwa madai kuwa mafundi na wasimamizi hao wameshindwa kutimiza wajibu na kusababisha miradi kutekelezwa chini ya kiwango.

Waliokumbana na rungu hilo ni fundi mkuu katika Shule ya Msingi Makatani iliyopo kijiji cha Ihumilo, Stephen Kayogo na fundi Mkuu wa mradi wa nyumba ya mtumishi katika Shule ya Msingi Nyamikoma, kijiji cha Lwenge, Mathayo Mgongo.

Wengine waliowekwa mahabusu wakidaiwa kutotimiza wajibu katika miradi hiyo inayotekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ni ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Emmanuel Masondole na mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa nyumba ya watumishi na vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Nyamikoma, Juma Richard.

“Pamoja na kutekelezwa chini ya kiwango, tumebaini usimamizi duni uliosababisha uharibifu wa mali ya umma, ikiwemo matumizi mabaya ya saruji na hivyo kuitia Serikali hasara,” alisema Shimo, huku akitoa muda wa siku 14 kasoro zote zilizobainika kurekebishwa

Naye Mratibu wa Tasaf wilayani hapa, Gabriel Evarist alisema ofisi yake inakamilisha mchakato wa kuvunja mikataba na baadhi ya makandarasi, akiwemo anayetekeleza mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Makatani ili kupata wengine wenye uwezo watakaokamilisha miradi hiyo kabla ya Agosti 22.

“Hatuwezi kuendelea nao kwa sababu hawaendi na kazi tunayoitaka, tutavunja mikataba yao ili tuone wanaoweza kufanya kile tunachokikusudia kwa wakati.

“Kuwepo kwao kwenye mradi kunaweza kutuchelewesha sana kwa sababu hawana haraka, nadhani tumalizane nao,” alisema.

Kwa upande wa Lucia Makono, mkazi wa kijiji cha Nyamikoma aliiomba Serikali na mamla nyingine husika kuongeza umakini katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili ubora ulingane na thamani halisi ya fedha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live