Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC awaonya wanaolalamika vyuma vimekaza

90022 Maisha+pic DC awaonya wanaolalamika vyuma vimekaza

Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mirerani. Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro (DC) mkoani Manyara nchini Tanzania, Zephania Chaula amewataka wanawake, vijana na wenye ulemavu kuacha kulalamikia maisha magumu wakati wameshindwa kuchangamkia fursa ya Sh230 milioni zilizotengenezwa kwa ajili ya mikopo.

Chaula aliyasema hayo jana Jumatano Desemba 25, 2019 kwenye tafrija ya sikukuu ya Krismasi ya watoto yatima, wanaoishi katika mazingira hatarishi, wenye ulemavu na wazee iliyoandaliwa na Charles Mnyalu mdau wa maendeleo wa mji mdogo wa Mirerani.

Alisema ni jambo la kushangaza kuona bado watu walalamikia hali nguvu au kudai vyuma vimekaza wakati kuna fursa ya mikopo imetolewa lakini jamii imeshindwa kuchangamkia fursa hiyo.

Alisema wanawake, vijana na wenye ulemavu wajiunge kwenye vikundi na kuvisajili kupitia ofisa maendeleo ya jamii ambaye atawasaidia kuwaandalia katiba ya vikundi bila kulipia gharama zozote.

"Na fedha zenyewe wala hazina riba endapo mkikopa Sh10 milioni mnarudisha Sh10 milioni hivyo changamkieni fursa hizo acheni kulalamika kuwa maisha magumu wakati ninyi wenyewe hamjatumia nafasi," alisema Chaula.

Amlisema kwa mwaka 2019 wanawake walitengewa Sh73 milioni na wakakopa S0h33 milioni, vijana walitengewa Sh72 milioni ila wakakopa Sh17 milioni na wenye ulemavu walitengewa Sh36 milioni.

Mkuu huyo wa wilaya alisema katika kata 18 zilizopo kwenye wilaya hiyo, kuna vikundi 1,212 vya wanawake, vikundi 23 vya vijana na vikundi vitatu pekee vya watu wenye ulemavu.

Mdau wa maendeleo wa mji wa Mirerani, Charles Mnyalu ambaye ndiye aliandaa tafrija alisema wamejumuika pamoja ili kuwapa furaha wahitaji.

Alisema kwenye tafrija hiyo wamefurahia pamoja na watoto yatima, wenye uhitaji maalum, wazee na walemavu wa mji mdogo wa Mirerani.

"Watu wasione sisi tuna fedha nyingi sana kwa kuandaa tafrija hii hapana, tumeona tufurahie pamoja na wahitaji hawa kama tulivyofanya kwenye sikukuu ya Idi," amesema Mnyalu.

Alisema pia wamegawa vifaa vya masomo kwa watoto hao ikiwemo madaftari, kalamu na nguo ili nao waone bado kuna wazazi wanawajali na kuwathamini hapa duniani.

Chanzo: mwananchi.co.tz