Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasri Ally amepiga malufuku kuongeza kiasi chochote cha fedha kwenye Viuatilifu aina ya Salfa vya zao la Korosho, vilivyosambazwa na Serikali Wilayani humo na Serikali kwa Wakulima. Khadija ameyasema hayo mjini Mkuranga, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Wajumbe wa Halmashauri kuu ya Chama hicho Wilaya akidai Viuatilifu hivyo hutolewa bure kwani ni ruzuku kutoka Serikalini vikilenga kumsaidia mkulima wa Korosho ili anufaike na kilimo.
Amesema, “hatutaki Mheshimiwa Rais agombanishwe na Wananchi wa Wilaya ya Mkuranga alitafuta fedha na akahakikisha Salfa inakuja bure, kwahiyo naomba tukayasimamie hayo katika Kata zetu na mkawaeleze Wakulima Salfa ni haki yao kuipata bila kutoa hata senti moja, hayo ndio maelekezo kutoka kwa Mheshimiwa Rais.”
Akizungumza kwa Njia ya simu Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wa Wakulima mkoa wa Pwani – CORECU, Musa Mng’eresa amesema kulikuwa na vyama vya msingi – AMCOS vitatu vya Kata ya Magawa Wilayani Mkuranga ambavyo viliwatoza gharama za usafiri Wakulima wakati wa kuchukua Salfa zao, lakini baada kupewa maelekezo waliacha.