Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu ameagiza makandarasi wa Shirika la Uchumi la jeshi la Kujenga taifa Suma JKT na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuimarisha jengo la utawala linavujisha maji kutokana na mvua zinazonyesha.
Buswelu amebaini tatizo hilo leo Novemba 8, 2021 wakati akikagua jengo hilo, akisema mpaka sasa ujenzi huo uliotakiw akukamilika Agosti mwaka huu, umeshakamilika kwa asilimia 80.
“Mkataba umeisha tulitegemea Mkurugenzi na watumishi wake wahamie hapa lakini bado. Sasa natoa maelekezo kwa taasisi tatu wakae siyo zaidi ya Ijumaa ya wiki hii, watazame sababu za jengo kuvuja. Kisha wahame kutoka kwenye majengo ya hospitali ili yatumike kutoa huduma za afya kwa wananchi,” amesema DC Buswelu.
Kwaupande wake msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Suma JKT, Gaspar Mwakipesile amekiri kuwepo tatizo la kuta kuvuja maji na kwamba tayari wameanza utatuzi wake.
“Upungufu huu wa kitaalamu kwenye ujenzi huwa unatokea. Kilichosababisha maji kuvuja ni kutokana na silabu iliyojengwa, kuna vitu havikuwekwa sawa ili kuepusha jambo hili, siyo kwamba vilisahauka.
“Tunajenga kwa hatua, tulianza kuweka marumaru na baadaye vinafuata vingine. Tatizo hili limesababishwa na kukimbizana na muda na mvua imetuonyesha wapi pakufanyia marekebishoi," amesema Mwakipesile.
Kuhusu mradi kuwa nje ya mkataba, amesema ni kutokana na sababu ambazo zipo pande zote ikiwamo upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kuwa mgumu.
“Tunanunua vifaa kutoka Dare es Salaam na kusafirisha inachukua muda, siyo kwamba ni uzembe wa wasimamizi. Mkoa huu haujafikia kiwango cha kuwa na huduma zinazohitajika.
“Mkataba ulikuwa wa miezi 18 tukaomba tukaongezewa miezi sita bado ukawa haujakamilika, tukaomba tena miezi sita ilichukua muda kujibiwa, hata hii tuliyoomba awamu hii hatujajibiwa,” amesema.
Jengo hilo litagharimu jumla ya Sh Sh3.6 bilioni litakapokamilika.