Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC avunja vibanda vilivyojengwa soko la Chifu Kingalu

Dc Sokoooo.png DC avunja vibanda vilivyojengwa soko la Chifu Kingalu

Fri, 15 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, amesimamia uvunjaji wa vibanda na makontena ya biashara yaliyowekwa kwenye maeneo ya wazi na kwenye soko kuu la Chifu Kingalu na Mawenzi yaliyopo Manispaa ya Morogoro.

Hatua hiyo imekuja baada ya kupata taarifa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji ya Manispaa ya Morogoro, Ally Kalungwana maarufu kama Ally Nyau kudaiwa kujenga kibanda kwenye eneo la wazi la soko la Chifu Kingalu na alipoagizwa kuvunja kwa hiari alikaidi agizo hilo.

Hata hivyo, alipoulizwa kwa simu kuhusu hatua hiyo, Kalungwana amesema hawezi kulizungumzia kwa kuwa hafahamu chochote.

Akizungumza wakati uvunjaji huo, mkuu huyo wa wilaya amesema hakuna mtu aliyekuwa juu ya sheria na kwamba kitendo cha mwenyekiti huyo wa kamati ya mipango miji ambaye pia ni diwani wa Mwembesongo ni kosa kama makosa mengine ya uvamizi.

"Awali eneo hili la wazi la soko kuu la Chifu Kingalu kuna watu waliiomba wajenge vibanda vya biashara, lakini kwa kutambua sheria inazuia hatukuwapa.

“Sasa leo hii mwenyekiti wa kamati ya mipango miji ambaye ni diwani anakuja kujenga hapa, hii inaleta picha gani? Lazima tuchukue hatua dhidi ya huyu diwani na hatua ya kwanza ni kuvunja na hatua nyingine ni kimfikisha kwenye vyombo vya nidhamu kwa kuwa anatumia vibaya madaraka yake," amesema Nsemwa.

Pamoja na kuvunja vibanda hivyo vya diwani huyo, pia mkuu huyo wa wilaya ameagiza halmashauri kutoa notisi kwa wamiliki wa vibanda na makontena yote yaliyowekwa maeneo ya wazi, ili wavunje wenyewe kwa hiari kwani watakapokaidi watachukulia hatua nyingine za kisheria.

Amesema soko hilo la Chifu Kingalu ni la kisasa na ujenzi wake umegharimu fedha nyingi, hivyo ni marufuku kuweka vibanda, makontena ama biashara yoyote kwenye maeneo ya wazi.

"Pale kwenye eneo la wazi jirani na soko la Mawenzi kuna kontena limewekwa kinyume cha sheria na wanaendelea na biashara za kuuza unga wa sembe, sasa naagiza lile kontena liondoke haraka na makontena mengine yote yaliyowekwa maeneo ya wazi yaondoke," amesema Nsemwa.

Ofisa tarafa wa Manispaa ya Morogoro, Winfred Kipako akiandika neno 'ondoa' kwa wino mwekundu kwenye kontena la biashara lililowekwa kwenye eneo la wazi lililopo jirani na soko la Mawenzi Manispa ya Morogoro. Picha Hamida Shariff

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Christopher Komba amekiri kupokea taarifa ya uvamizi wa eneo la wazi la soko kuu Kingalu uliofanywa na diwani huyo, hivyo walitoa notisi ya kumtaka avunje mwenyewe kwa hiari hata hivyo hakutekeleza.

"Ni kweli tulipata taarifa ya ujenzi wa vibanda hivi kwenye eneo la wazi la soko la Chifu Kingalu, tulifika hapa na kukuta ujenzi ukiendelea, tukatoa zuio na kumtaka aliyewekeza hapa avunje mwenyewe lakini hakuvunja, nashukuru leo mkuu wa wilaya pamoja na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya amekuja kusimamia zoezi hili la uvunjaji," amesema Komba.

Akitoa taarifa ya uvamizi wa maeneo ya wazi ya soko kuu la Chifu Kingalu, mwenyekiti wa soko hilo, Kharid Mkunyegele amesema baada ya kuona ujenzi wa vibanda hivyo, uongozi wa soko ulitoa zuio lakini ujenzi uliendelea, hivyo waliandika barua kwenda manispaa ili kupata nguvu ya kuzuia ujenzi huo.

Amesema baada ya kupeleka taarifa halmashauri juu ya uvamizi huo, waliona pia wafikishe taarifa hizo kwa mkuu wa wilaya.

Mmoja wa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya wazi yaliyovamiwa, Mariamu Salumu amesema uvamizi huo umekuwa ukisababisha baadhi ya shughuli za kijamii zinazopaswa kufanywa kwenye maeneo hayo zikwame na pia watoto kukosa mahala pa kucheza.

"Watoto wanagongwa na bodaboda kwa sababu wanacheza barabarani, kwa kuwa wamekosa maeneo ya kucheza, mikutano ya hadhara, mikutano ya mtaa tunafanyia kwenye baraza za watu wakati maeneo haya ya wazi ndio yanatakiwa yatumike," amesema Mariamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live