Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC atoa siku 14 waliovamia wilayani kwake kuondoka

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Zanzibar. Wilaya ya Kaskazini B imetoa wiki mbili kwa wahamiaji kutoka nje ya wilaya hiyo wanaoishi kinyume cha utaratibu kuondoka haraka kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

Wahamiaji hao wanaoishi eneo la Kiwengwa wametakiwa kurejea walikotoka hadi watakapokamilisha utaratibu halali wa uhamiaji katika shehia hiyo.

Agizo hilo lilitolewa jana na mkuu wa wilaya ya Kaskazini ‘B’, Rajab Ali Rajab, alipokuwa kwenye operesheni maalumu iliyopewa jina la ‘Safisha Kiwengwa’ kutokana na kukithiri kwa wahamiaji wanaodaiwa kujishughulisha na vitendo viovu vya ukahaba, ulevi na uporaji.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wameamua kufanya operesheni hiyo baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wakazi wa eneo hilo, wakilalamika kukithiri kwa vitendo vya uhalifu vinavyodaiwa kufanywa na wageni, hali inayowafanya waishi kwa hofu.

“Eneo la Kiwengwa ni muhimu kwa Serikali katika kuingiza pato kwa kuwa ni la kitalii, hivyo baadhi ya vitendo vinavyofanywa vinasababisha mmomonyoko wa maadili,” alisema Rajab.

Hata hivyo, Rajab ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo alisema, zaidi ya watu 50 wamekamatwa katika operesheni hiyo, huku akiahidi kamati hiyo itaendeleza msako huo ili kutokomeza vitendo hivyo na kurudisha heshima ya watu wa Kiwengwa.

Aidha, alisema anakusudia kufanya operesheni maalum nyingine kwa lengo la kudhibiti vijana na watu wa kabila la Wamasai ambao mara nyingi wamekuwa wakifanya vurugu wakiwa wanatembea na silaha za jadi.

Katibu wa Sheha wa shehia hiyo, Vuai Juma Kondo, alikiri kuwapo kwa wahamiaji wasiofuata taratibu za uhamiaji na kusababisha usumbufu kwa uongozi.

Alisema uwapo wa wahamiaji hao ni miongoni mwa sababu za ongezeko la matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwamo wizi aliodai unafanywa na wageni.

Alisema mara nyingi amekua akipokea kesi zinazowahusu wahamiaji hao ikiwamo kufanya fujo na kupigana kwa kutumia silaha za jadi.

Alisema wakati sasa umefika kila anayeishi eneo hilo kuzingatia sheria na maadili mwema.

Chanzo: mwananchi.co.tz