Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC atoa onyo kwa madaktari wanaowapa wanafunzi dawa za uzazi wa mpango

38406 Dcpic DC atoa onyo kwa madaktari wanaowapa wanafunzi dawa za uzazi wa mpango

Tue, 29 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ruangwa. Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa amesema mhudumu yeyote wa afya atakayebainika kumpa dawa za uzazi wa mpango mwanafunzi wa kike atachukuliwa hatua za kisheria.

Pia, amewataka wanaume wanaopigwa na wake zao kuripoti masuala hayo katika vyombo vya dola.

Akizungumzia suala la wanafunzi kupewa dawa za mpango wa uzazi, alisema hata mwanafunzi atakayekutwa anachoma sindano au njia nyingine za mpango huo atahesabiwa kuwa ni mhalifu na atachukuliwa hatua.

Mgandilwa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake, Ruangwa mkoani Lindi.

Alisema, “Juzi nilitembelea zahanati ya Mibule na moja ya mambo ambayo nimeyachukulia hatua kupitia kwa mkurugenzi (mtendaji wa halmashauri ya wilaya) na mganga mkuu wa wilaya ni hilo la watoto wa kike kutumia sindano za uzazi wa mpango.”

Alisema ameiagiza ofisi ya mganga mkuu kutoa maelekezo na kuandika barua za miongozo kwenye hospitali, zahanati, wauguzi na waganga wote kuacha mara moja kuwapa dawa za uzazi wa mpango watoto wa kike wenye umri wa chini ya miaka 18. “Niendelee kutoa wito kwa madaktari, huu uzazi wa mpango upo kwa ajili ya watu wenye rika linaloruhusiwa na siyo kwa wanafunzi. Na nyinyi wanafunzi malizeni shule na hayo mambo mengine ni baadaye,” alisema.

Alisema kumpa dawa za uzazi wa mpango mtoto wa kike ni kumruhusu kwenda kutumika.

Wiki iliyopita Mwananchi lilichapisha habari iliyobainisha jinsi wazazi katika kata ya Nambilanje wilayani humo wanavyowachoma watoto wao wa kike wenye umri wa kuanzia miaka 11 sindano za uzazi wa mpango.

Mwananchi liliyaibua hayo baada ya kufanya uchunguzi na kuzungumza na wazazi, wanafunzi, walimu na baadhi ya viongozi wa kata hiyo. Pamoja na kupiga marufuku watoto wa kike kuchoma sindano za uzazi wa mpango, pia Mgandilwa aliwataka wanaume wanaopigwa na wake zao kutoa taarifa kwenye madawati ya jinsia yaliyo karibu nao. “Hakuna aliyeruhusiwa kupiga mtu, iwe ni mwanamke au mwanaume kama amepigwa anahitaji kutoa taarifa kwenye dawati la jinsia,” alisema.

Alisema kuna wakati mwanamume anaweza kupigwa halafu akajificha, lakini anakuwa hajitendei haki.

Akizungumza wakati wa mafunzo kwa wanakamati za ulinzi wa wanawake na watoto juzi, yaliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), mtendaji wa kata ya Likunja, Hassan Kalembo alisema anapokea malalamiko mengi ya wanawake kuwapiga waume zao.

“Hizo ni zile ambazo zimeripotiwa, zipo nyingi ambazo wanaume wanapigwa lakini hawaripoti,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz